Kwa mara nyingine tena, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi, umeshuhudia hitilafu za umeme.
"Takriban saa mbili Jumamosi usiku, JKIA ilipata hitilafu katika usambazaji wa umeme kutokana na kukatika kwa gridi ya taifa." KAA iliandika kwenye kurasa zake mtandaoni.
Hata hivyo, mamlaka hiyo ya viwanja vya ndege Kenya (KAA) imesema, ilirekebisha hitilafu hiyo ndani ya muda mfupi na shughuli za kawaida zilirejea uwanjani humo.
"Jenereta za ziada za uwanja wa ndege zilianzishwa, na kurejeshwa kamili kwa nguvu kutokea ndani ya dakika 8 - 20.'' KAA iliandika.
"Vifaa vyetu vingine vilirudisha usambazaji wao wa umeme kwa muda mfupi sana."
Mamlaka hiyo imeomba radhi kwa tukio hilo.
"KAA imejitolea kudumisha shughuli zisizokatizwa na inajutia usumbufu wowote kwa abiria na washikadau uilotokana na kukatika kwa umeme."
Hata hivyo, wakenya kwenye mitandao ya kijamii walionekana kutofurahishwa na tukio hilo la ukosefu wa umeme huku wakitoa wito kwa serikali kurekebisha hali hiyo ya mara kwa mara.
Mwezi Agosti kisa kama hiki kilitokea katika uwanja huo na maeneo mengine nchini ambapo umeme ulikatika kwa saa kadhaa na kutatiza usafiri.
Kutokana na tukio hilo waziri wa usafiri Kipchumba Murkomen aliwaomba radhi Wakenya na kuwahakikishia haitajirudia tena.
Isitoshe waziri huyo alifanyia mabadiliko makubwa bodi ya usimamizi ya halmashauri ya safari za ndege Kenya KAA, ikiwemo kuwahamisha wakurugenzi wa viwanja mbali mbali vya ndege na kuwashusha wengine vyeo.