Waziri wa usafiri nchini Kenya Kipchumba Murkomen amejitokeza kuomba radhi kwa wasafiri waliohangaishwa na ukosefu wa umeme nchini n akuathiri shughuli katika uwanja wa ndege wa kimatafa JKIA Ijumaa usiku.
"Ninasikitika sana kwa kile kilichotokea JKIA na kukatika kwa umeme," Waziri Murkomen alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter. "Hakuna kisingizio cha kuripoti na hakuna sababu kwa nini uwanja wetu wa ndege uko gizani."
Umeme ulikatika kwa muda wa saa tano kuanzia saa tatu na robo saa za Afrika Mashariki na kuwaacha wasafiri wengi wakihangaika.
Hakuna ripoti iliyotolewa juu ya safari ngapi zilikatishwa kutokana na hitilafu hii.
''Tulipata hitilafu katika mifumo yetu ya kusambaza umeme na kusababisha upotevu wa umeme kwa wingi sehemu mbalimbali nchini.'' Shirika la Umeme nchini KPLC ilisema katika mtandao wake wa X. ''Tunaomba radhi kwa wateja wetu kwa usumbufu uliojitokeza.'' iliendelea kusema taarifa hiyo.
Asubuhi waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen naye aliandika katik amtandao wake kuwa amewasili uwanja huo wa ndege kujua chanzo cha usumbufu huo huku akihakikisha kuwa hautatokea tena.
Uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi ni miongoni mwa viwanja vyenye shughuli nyingi zaidi barani Afrika huku ikikadiriwa kutua ndege zaidi ya 150 kwa siku.
Data ya Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) katika Utafiti wake wa Kiuchumi wa 2022, inaonyesha kuwa idadi ya abiria waliohudumiwa katika viwanja vya ndege vya Kenya wengi wao kupitia JKIA, ilipanda kwa kiasi kikubwa kutoka abiria milioni 6.7 mwaka wa 2021 hadi abiria milioni 10.2 mwaka wa 2022.