Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wa nchini Tanzania (JNIA) umetambuliwa kama moja ya viwanja vya ndege salama zaidi kwa matumizi duniani.
Kwa mujibu wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (ACI), JNIA ni kati ya viwanja vya ndege vinavyothamini usalama wa watumiaji wake, katika Mkutano Mkuu wa 33 wa ACI Africa, uliofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini, Septemba 20, 2024.
“Tuzo hii ni dhihirisho tosha la utayari wetu wa kuimarisha usalama kwa watumiaji wa kimataifa wa uwanha huu,” amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi nchini Tanzania, Profesa Godius Kahyarara.
Kulingana na Profesa Kahyarara, Tanzania imeorodheswa katika kipengele namba moja kati ya mataifa yenye kukidhi vigezo vya usalama vya Shirika la Usalama wa Anga Duniani (ICAO), huku likiwa na idadi ya miruko zaidi 40,000 ya ndege kila mwaka.
Tuzo hiyo ya heshima, hutolewa kwa viwanja vya ndege wa kimataifa ulimwenguni vinavyothamini usalama wa watumiaji wa viwanja hivyo, kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
JNIA ni kiwanja cha ndege kikubwa na muhimu zaidi nchini Tanzania, kikiwa kipo kilomita 12 kutoka kitovu cha jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Kilipewa jina hilo kama heshima kwa Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.