Kulingana na EWURA, gharama ya nishati ya petroli katika bandari ya Dar es Salaam imepungua kutoka Dola 1.11 (Shilingi za Kitanzania 3,011) kwa lita kwa mwezi Oktoba hadi Dola 1.08(Shilingi za Kitanzania 2,943) kwa mwezi wa Novemba./Picha:Getty

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), imesema kuwa gharama za nishati ya petroli zimepungua kutoka Dola 1.11(Shilingi za Kitanzania 3,011) kwa mwezi Oktoba, hadi dola 1.08 (Shilingi za Kitanzania 2,943) mwezi Novemba, kwa watumiaji wa mkoa wa Dar es Salaam.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Novemba 6, 2024, mamlaka hiyo imesisitiza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na mwenendo wa gharama za uagizaji na viwango vya kubadilisha fedha za kigeni.

“Gharama za uagizaji wa mafuta zimepungua kwa wastani wa asilimia 3.91 kwa petroli na kuongezeka kwa asilimia 14.48 kwa dizeli, huku kukiwa hakuna mabadiliko kwenye mafuta ya taa,” EWURA imesema.

Kulingana na mdhibiti huyo, kwa gharama za mwezi Novemba 2024, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 1.75.

“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” taarifa hiyo imeongeza.

Aidha, EWURA imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

TRT Afrika