Ray C amewahi kushinda tuzo nyingi za muziki zikiwemo; tuzo ya Msanii bora wa kike mwaka 2004. /Picha: Rayctanzania/ IG 

Na Paula Odek

Ray C, alizaliwa Mei 15, 1984 ana asili ya mkoa wa Iringa nchini Tanzania na alianza kama mtangazaji wa East Africa Radio kabla ya kuhamia Clouds FM, zote za jijini Dar es Salaam.

Mwaka 2003, Ray C, au ‘Kiuno Bila Mfupa’ kama alivyojulikana na mashabiki wake, aliachia albamu yake ya kwanza iliyoitwa “Mapenzi Yangu”, ambayo ilikuwa na nyimbo kali kama vile Sikuhitaji, Mapenzi Yangu, Nawewe Milele, Ulinikataa bila sababu, Mahaba ya dhati na Uko wapi?

Mwaka uliofuata, Ray C akatoa albamu nyingine iliyoitwa Na wewe Milele kisha ikafuata Sogea Sogea ya mwaka mwaka 2006 kabla ya kuachia Touch Me mwaka 2008.

Ray C amewahi kushinda tuzo nyingi za muziki zikiwemo; tuzo ya Msanii bora wa kike mwaka 2004, Msanii bora wa kike Afrika Mashariki mwaka 2004 kupitia KISIMA MUSIC AWARDS na Msanii bora wa kike mwaka 2007 kupitia TMA tena.

Pia amewahi kuwania tuzo za za kimataifa kama vile Pearl of Africa Music Award kwa mwaka 2006 na Channel O Music Awards mwaka ya mwaka 2005.

Ray C anabakia kuwa kati ya wasanii waliopendwa zaidi na kila rika kutokana na muonekano wake na aina yake ya kucheza, ni msanii aliyekuwa na mvuto zaidi pia muonekano mzuri.

Aliwahi kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na aliyekuwa mshiriki wa shindano la Big Brother Africa, Mwisho Mwampamba kutoka Tanzania.

Pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na rapa Lord Eyez kutoka Tanzania, kabla hajatumbukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa muda mrefu.Kwa kauli yake mwenyewe, Ray C anasema kuwa aina ya marafiki aliokuwa nao ndiyo walimfanya kuingia kwenye matumizi hayo.

Msanii huyo alizama kwenye uraibu wa dawa za kulevya kabla ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, kumsaidia na kumpeleka kwenye kituo maalumu cha kuwasaidia waathirika wa dawa hizo.

Licha ya kupona uraibu huo, haikuwa tena rahisi kwa Ray C kurudi tena kwenye gemu ya muziki.

Alimua kuanzisha taasisi ya Ray C Foundation kwa lengo la kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na miaka michache baadaye akaelekea nchini Ufaransa ambako anaishi mpaka sasa, akiwa amejaliwa kupata mtoto mmoja aitwaye Shahrukh.

Katika mahojiano yake aliyofanya mwaka 2024, Ray C alisema kuwa anatamani kurudi Tanzania, japo roho yake inasita, na kwamba anapachukia kutokana na mambo aliyopitia akiwa nchini humo.Kwa maneno yake mwenyewe, anasema kuwa anajisikia salama na amani zaidi akiwa Ulaya kuliko kurudi nchini Tanzania.

TRT Afrika