Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba nchini Uganda, imeomba bunge kuwaruhusu mawakili wa serikali kutolipa kodi ya mapato.
Waziri Nobert Mao amesema hii itapunguza pengo la tofauti ya mishahara kati ya mawakili wa serikali na wenzao waendesha mashtaka katika Ofisi ya Kurugenzi ya Mashtaka (ODPP) na Mahakama.
“Ofisi ya DPP haikabiliwi na tatizo kama hilo kwa sababu wameondolewa ushuru wa mapato, hivyo wanapata malipo bora,” alisema Mao.
“Tunataka hivyo hivyo kwa Mawakili wa Wizara ya Sheria ili nao wapewe malipo ya ushindani na waache kutafuta kazi nje. Kila mwaka, tunapoteza baadhi ya mawakili wetu bora, na bado tumewekeza katika kuwafundisha na ghafla, wanaenda Mahakama Kuu kwa sababu sheria na masharti ni bora zaidi. Hii inaathiri ubora wa kazi zetu,” aliongeza Waziri Mao.
Hata hivyo, Fox Odoi mbunge wa Budama Kaskazini bado anazungumza juu ya tofauti ya malipo kwa kazi hiyo hiyo, wakati yeye mwenyewe anakaa kwenye Baraza la Mawaziri ambalo linakuja na sera hizi.
"Tunaongelea mwaka 2025, Waziri anasema kuwa ana wanasheria katika ODPP ambao wanalipwa zaidi ya wanasheria katika kitengo cha wanasheria wa serikali, kazi sawa, malipo tofauti," Odoi alisema.
Kesi za serikali
Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema timu yake ilishinda kesi 311 mahakamani na hapo serikali ikaokoa zaidi ya dola milioni 758 ( UGX2.8Trn).
Serikali pia ilipoteza kesi 101 zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 48 (UGX179.4Bn) mnamo 2024.
"Pia tuliweza kuitetea Serikali katika kesi 180 za Kikatiba, Rufaa na Maombi katika Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Robert Kasande, Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba ya Uganda.
Hata hivyo, Jonathan Odur mbunge wa Erute Kusini aliitaka Wizara kueleza ni kiasi gani cha fedha kwa kesi iliyoshindwa zimerejeshwa na Serikali.
"Serikali imeshinda kesi nyingi, inapata mapato kutokana na juhudi hizo kwa sababu watu wameishtaki serikali imeshindwa, kwao wanapokea malipo ya fidia. Tunataka kuona takwimu za mapato yenu," Odur alisema.