Viatu vilivyotenezwa nchini Kenya vimekumbana na upinzani mkubwa kutoka vinavyotenezwa nje ya nchi. Picha:  Reuters

Kenya imeazimia kupiga marufuku uingizwaji wa viatu kutoka nje ya nchi hatua inayotazamiwa kukuza uzalishaji wa ndani, Rais William Ruto amesema.

Mpango huo unafuatia juhudi za mwaka mzima za serikali ya Kenya katika kufungua uwezo wa kiviwanda katika tasnia ya uchomaji ngozi katika nchi hiyo yenye mifugo mingi ya Afrika Mashariki.

"Mpango huo ni muhimu katika mkakati wetu wa kufanya mapinduzi katika mnyororo wa thamani wa ngozi kutoka ule unaoendeshwa na mauzo ya nje ya malighafi na bidhaa zilizosindikwa nusu hadi sekta ya kisasa," Ruto alisema katika hotuba yake Jumamosi wakati wa sherehe za siku ya Madaraka, ambapo ni sherehe ya kukumbuka nchi hiyo ilivyoweza kujitawala kutoka kwa Waingereza.

Alisema kuwa serikali ya nchi hiyo inaendeleza uwezo wa nchi hiyo kutengeneza malighafi ya bidhaa za kutengeneza viatu.

"Nimejiwekea ahadi kuwa ndani ya kipindi kifupi, tutaacha kuagiza viatu kutoka nje. Tutaanza kuvaa viatu vilivyotengenezwa nchini Kenya kwa kutumia ngozi zetu wenyewe," alinukuliwa na tovuti ya chombo cha habari cha Citizen.

Viatu vya mtumba

Kaya nyingi nchini Kenya hupenda kuvaa viatu vya mitumba kutoka nje ya nchi ambavyo huwa ni vya bei nafuu na kuwa na ubora wa juu.

Bidhaa za ngozi zinazozalishwa ndani ya nchi huhusishwa na utajiri.

Katika risala yake, Ruto alisema kuwa dola milioni 3 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha sekta ya ngozi nchini humo. Fedha hizo zitatumika katika kununua mashine za kisasa na kujenga kiwanda cha viatu.

Hifadhi ya viwanda vya ngozi pia inajengwa viungani mwa mji mkuu, Nairobi, ambapo ekari 100 za ardhi zitatengwa kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya ngozi.

TRT Afrika