Na Lulu Sanga
Shirika la Afya ulimwenguni limetangaza rasmi ukomo wa hali ya dharura ya kimataifa ya UVIKO-19 hapo jana siku ya Ijumaa ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu baada ya tamko lake la awali juu ya hatari ya ugonjwa huo mnamo January 2020.
“Kwa matumaini makubwa tunatangaza mwisho wa Uviko-19 kama dharura ya afya ya uma ulimwenguni” ametangaza Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) huku akisisitiza kwamba “haimaanishi ugonjwa huo sio tishio tena ulimwenguni”.
Ni mengi yamejiri na kutokea katika kipindi hicho chote ambapo Afrika na Dunia kwaujumla imepambana kukabiliana na ugonjwa huo uliosababisha vifo vya Zaidi ya watu milioni 6.
Lakini je ni yapi tumejifunza kutokana na janga la Corona?
Nchi za Afrika kuboresha mfumo wake wa afya katika hospitali binafsi na za serikali.
Suala la upatikanaji wa huduma za afya ni suala nyeti na la msingi Zaidi.
Tumeshuhudia watu wakienda hospitali na kurudishwa majumbani kutokana na sababu mbali mbali. Huenda wahudumu ni wachache kuliko idadi kubwa ya wagonjwa. Baadhi ya nchi na maeneo watoa huduma walikua hatarini Zaidi kwani kulikua na ukosefu mkubwa wa vifaa tiba.
Upatikanaji wa dawa wakati wa janga la Uviko 19 ilikua ni moja ya shida kubwa kwani hospitali nyingi za uma katika nchi mbalimbali barani Afrika zilikuwa zinakabiliwa na uhaba wa dawa na matatizo ya upatikanaji wa oksijeni katika kila hospitali binafsi na za serikali.
Kwa mujibu wa tathmini ya WHO ya uwezo wa kukabiliana na milipuko, kaunti nyingi za Kiafrika ziliathiriwa sana wakati wa janga la Uviko 19. Kulikuwa na uhaba wa vitanda vya wagonjwa mahututi, uwezo mdogo wa maabara na changamoto nyingine nyingi.
Lakini kukabiliana na yote haya nchi za Afrika zinajukumu kubwa la kufanyia kazi upya sera za afya ya uma.
Dawa za asili mitishamba ni Lulu ya Afrika
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani dawa za asili ndio chanzo pekee cha huduma za afya kwa asilimia 80 ya watu barani Afrika. Na hii inatokana na upatikanaji wake lakini pia hazina gharama ukilinganisha na dawa za kisasa.
Katika kipindi ambacho janga la Uviko-19 limeishambulia Dunia, wakazi wa nchi mbali mbali za Afrika waligeukia tena mitishamba ambayo awali ilitumiwa Zaidi na wale wanaoishi maeneo ya vijijini.
Kujifukiza kwa kutumia mimea ya asili iliyochemshwa kwapamoja ni njia iliyopewa uzito mkubwa na baadhi ya nchi za Afrika hasa Tanzania ambapo pamoja na kutumiwa dawa za hospitali kuliwekwa vituo vya uma ili watu waweze kukabiliana na Uviko kwa kujifukiza kiasili.
Mbinu hii iliwapa ahueni wengi na ilitumiwa hata na waafrika waliokua wakiishi ughaibuni.
Kwa kutumia mizizi, matunda na majani ya mimea mbalimbali wataalamu wa tiba asilia katika nchi mbalimbali walitengeneza dawa ambazo baadhi ziliidhinishwa na maabara za kitaifa za nchi husika.
Kwa mustakabali huo nchi kama Madagascar, Tanzania, Kenya, Uganda ziliidhinisha tiba mbadala ya dawa za asili kukabiliana na Uviko 19. Kwa ktengeneza dawa mbalimbali zilizotumika katika kipindi chote cha janga la uviko-19
Lakini la muhimu hapa ni kuwa na kiasi na kutumia wataalamu wa kweli wa mitishamba badala ya watu kujitengenezea dawa kienyeji.
Mnamo Julai 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika walizindua kamati ya wataalam kusaidia nchi za Kiafrika katika matumizi ya dawa za asili dhidi ya virusi vya corona.
Utajiri afya pesa ni ziada
Utajiri mkubwa ni bure bila kuwekeza katika afya. Jamii imekuwa ikihimiza sana katika kuwekeza fedha, kuimarisha uchumi ilimradi upambane na umasikini.
Lakini katika kipindi cha janga la Uviko-19 Afrika na dunia imepata jambo la kiujifunza. Unaweza kuwa na mali nyingi lakini zisikusaidie katika kukabiliana na majanga hasa janga lenyewe linapopiga afya yako.
Uwezo wa kwenda ughaibuni kutibiwa upo lakini mipaka imefungwa, walioko ughaibuni nao wamezidiwa wanatafuta matibabu unayotafuta kwani hata wao wanapambana na unachopambana nacho.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani mpaka kufikia mwezi November 2022 zaidi ya watu 200000 waliaga dunia. Idadi hiyo haijazingatia uwezo wa mtu kwani hapo kuna matajiri na watu maarufu ambao pia walipoteza maisha.
Wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza sana kuwekeza katika afya, kampeni za kufanya mazoezi ya pamoja katika nchi za Afrika zimeongezeka. Mashindano ya mara kwa mara ili kuhamasisha watu kufanya mazoezi yanaendelea kila nchi.
Kula mlo sahihi ni miongoni mwa mambo ya msingi katika kuwekeza katika afya. Kipindi cha kukabiliana na janga dawa za vitamin C zilitolewa kwa wingi huku wataalamu wa afya wakisisitiza kula matunda na mboga za majani kwa wingi.
Je unakula mlo sahihi hasa matunda na mboga mboga kama wataalamu wanavyo elekeza au ni kusubiri mpaka maelekezo ya hospitali ukiumwa?
Hivyo sasa imebaki jukumu lakila mmoja wakati unakimbizana kupata utajiri na mali ili kuwezesha famili basi kimbizana kuimarisha afya yako nay a familia.
Kuwa na akiba ya Kutosha ya chakula
Je unakiasi gani cha hifadhi ya chakula nyumbani kwako? Nchi za afrika zina akiba kiasigani ya chakula kutosha hitaji la wananchi wao?
Wengi tunaamini akiba ni fedha lakini si kweli tumeona pesa ikishindwa kuwasaidia watu kupata chakula katika kipindi ambacho dunia inapambana na janga la Uviko-19.
Baadhi ya maeneo maduka na masoko yalifugwa chakula katika maduka makubwa kilikuwa cha kugombaniwa. Huku mahala pengine wenye uwezo walionekana kujilimbikizia. Na ghala ya siri yaliyofichwa chakula yaligunduliwa katika baadhi ya nchi kama Nigeria.
Serikali zilikemea lakini hofu ya njaa haikuzuia watu kujilimbikizia na bei kupandishwa kupita kiasi.
Akiba inaumuhimu wake haipaswi kusubiri janga ndio tuweke akiba.
Lakini pia Serikali za Afrika zina akiba kiasi gani kukabiliana na majanga kama haya? Je kiasi kilichopo kitadumu kwa muda gani?
Kuwa na vyanzo vya ziada vya mapato si kutegemea ajira pekee
Makampuni binafsi na ya serikali yalifungwa huku mashirika nayo baadhi yakifungwa. Sasa je nini kinafanyika baada ya hapo.
Baadhi waligeukia biashara za mtandao wengine walitumia fursa kutengeneza maudhui katika mitandao ya kijamii na kuwafariji wengi waliokua majumbani kwani hata baadhi ya maofisi yaliyoendelea na kazi watu walitekeleza majukumu wakiwa nyumbani.
Fursa nje ya ajira ni nyingi muhimu ni kupata ujuzi ambao unaweza kukuongezea uwezo wa kuzalisha hata ukiwa katika ajira.
Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani ILO, kufikia 2022 pekee Zaidi ya watu milioni 13.5 walipoteza ajira zao kutokana na janga la uviko-19 na hiyo ni kusini mwa jagwa la sahara pekee.
Na kuongeza kuwa Uwiano wa ajira kwa idadi ya watu (EPR) barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara umepungua kwa asilimia mbili kutokana na janga la COVID-19, ILO ilibainisha.
Kukemea na kudhibiti habari potofu kwa haraka.
Mitandao ya kijamii inanguvu kubwa pia imebeba faida endapo ikitumiwa vyema.
Lakini mengi hufanyika kwa lengo la kupotosha. Taarifa mbalimbali zakupotosha zilisambaa wakati wa janga hili. Picha za video miili ikizagaa kila mahali watu wamekufa zilikuwa zinatumwa huku baadhi zikikosa uhalisia. Habari za viongozi kuigiza wanapata chanjo pia zilisambaa.
Tumeona taarifa zinazo potosha kuhusu baadhi ya dawa na matumizi yake, tiba za kubuni mitandaoni ambazo hazijaidhinishwa na shirika la afya duniani, hali iliyozua hofu na kupelekea hata baadhi kupoteza maisha kwa uoga hata kabla ya kupata madhila ya ugonjwa wenyewe.
Si kila taarifa inayosambazwa mtandaoni inaukweli ni muhimu kuwa makini au kutumia wataalamu ili kupata uhalisia wenyewe.
Ugonjwa wa Uviko-19 iliotangazwa tishio kwa ulimwengu tangu mwaka 2020 imesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 6.9 pamoja na magonjwa mengine ya kudumu.
Nchi za Afrika bado zinanafasi kubwa ya kujifunza namna ya kukabiliana na majanga kama haya na kujikita katika uzalishaji wa Dawa na chanjo jambo linalo wezekana.