Chanjo ya kwanza ya MVA-BN imewasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC/ Picha: Reuters

Shirika la Afya Duniani, WHO kwa mara ya kwanza, imeidhinisha chanjo ya Mpox, hatua inayotarajiwa kuharakisha upatikanaji chanjo ili kupambana na janga linaloendelea barani Afrika.

Tangazo hilo lilikuja siku ya Ijumaa baada ya kuwasili kwa chanjo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

"Kuanza kwa chanjo dhidi ya Mpox ni hatua muhimu katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huo, katika muktadha wa milipuko ya sasa barani Afrika, na katika siku zijazo," alisema Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.

"Sasa tunahitaji kuwe na ongezeko la haraka katika ununuzi, michango na usambazaji ili kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo pale zinapohitajika zaidi... ili kuzuia maambukizi, kukomesha maambukizi na kuokoa maisha."

Kurahisisha ufikiaji

Mwongozo wa WHO unatumika kutathmini ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za matibabu kama vile chanjo, kuandaa njia kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa kuzinunua.

Mwongozo huo pia unatumiwa na nchi za kipato cha chini bila njia ya kufanya tathmini zao ili kuharakisha uidhinishaji wa ununuzi.

"Uhakikisho wa WHO wa chanjo ya MVA-BN utasaidia kuharakisha ununuzi unaoendelea wa chanjo ya mpox na serikali na mashirika ya kimataifa ... kwenye mstari wa mbele wa dharura inayoendelea barani Afrika na kwengineko," alisema Yukiko Nakatani, Mkuu Msaidizi wa WHO anayehusika na matibabu.

Mpox, ambayo awali ilijulikana kama Monkeypox, husababishwa na virusi vinavyopitishwa kwa wanadamu na wanyama walioambukizwa lakini pia inaweza kupitishwa kati ya binadamu kwa kukaribiana kimwili.

Mpox husababisha homa, maumivu ya misuli na vidonda vikubwa vya ngozi kama majipu, na wakati mwengine inaweza kuwa mbaya.

WHO ilitangaza dharura ya kimataifa kuhusu Mpox mwezi uliopita, ikisikitishwa na kuongezeka kwa idadi maambukizi aina mpya ya Clade 1b nchini DRC ambayo yalienea katika nchi za karibu.

DRC imerekodi takriban maambukizi 22,000 na vifo 716 vinavyohusishwa na virusi hivyo tangu Januari.

Hadi sasa, baadhi ya dozi 200,000 za chanjo zimefikiswha DRC na Umoja wa Ulaya, pamoja na takriban 50,000 kutoka Marekani.

TRT Afrika