Aliyekuwa waziri wa Mawasiliano Margaret Nyambura amekataa uteuzi wa nafasi ya balozi nchini Ghana. Picha/ kutoka kwa wengine. 

Aliyekuwa waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, ICT, Margaret Nyambura Ndung’u amekataa uteuzi wa Rais William Ruto kama balozi wa Kenya nchini Ghana akitaja sababu za kifamilia.

Rais William Ruto wa Kenya alimteuwa katika nafasi hiyo ya ubalozi Novemba 19, 2024.

Ndung’u alipangiwa kufika mbele ya Kamati ya bunge ya Ulinzi, Ujasusi na Mambo ya Nje ili kuhojiwa Ijumaa saa tatu asubuhi, lakini badala yake alituma barua kueleza rasmi uamuzi wake.

"Ningependa kutoa shukrani zangu kwa mwaliko wa kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mambo ya Nje mnamo Januari 10, 2025, katika jengo la Bunge la Nairobi," ilisema sehemu ya barua ya Ndung'u.

"Hii imesababishwa na masuala binafsi na ya kifamilia ambayo baada ya kuzingatia hayo sitoweza kuwa balozi nchini Ghana kama nilivyoteuliwa na Rais William Ruto mnamo Novemba 19, 2024," iliongezea.

Hii sio mara ya kwanza kwa nafasi hiyo ya ubalozi wa Ghana kukataliwa. Aprili 2024 Rais William Ruto alimteua aliyekuwa mbunge wa Mugirango Magharibi Victor Mogaka Kemosi lakini nae aliikataa.

Nyambura Ndung'u aliondolewa katika baraza la mawaziri katika mabadiliko ya hivi majuzi na Rais William Ruto ambaye wakati huo huo alimteua mnamo Disemba 24, 2024 kuwakilisha Kenya nchini Ghana.

Alihudumu katika wizara ya ICT kwa miezi minne.

TRT Afrika