Ghasia za magenge zimeongezeka kote Haiti, na zaidi ya watu 8,400 wameripotiwa kuuawa, kujeruhiwa au kutekwa nyara kwa jumla mwaka jana, zaidi ya mara dufu ya idadi iliyoripotiwa mnamo 2022.
Ziara ya Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry Kenya inalenga kusisitiza umuhimu mkubwa wa ujumbe wa msaada wa kiusalama kwa serikali ya Haiti, ambayo inatafuta suluhu ya haraka kuondoa magenge yenye silaha na kuhakikisha usalama wa raia wake.
Mbali na hayo, zaidi ya watu 310,000 wameachwa bila makazi kwani magenge yanakadiriwa kudhibiti hadi 80% ya mji mkuu wa Port-Au-Prince yakiendelea kupigana juu ya eneo.
"Waziri Mkuu atasafiri kwenda Nairobi, Kenya, kutamatisha mpango wa kupelekwa kwa vikosi vya pamoja vya usalama wa kimataifa maarufu MSS na mamlaka ya Kenya na zile za nchi nyengine katika bara la Afrika," Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema katika barua.
Ujumbe huo maalum wa usalama uliombwa na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry mnamo Oktoba 2022 na kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka mmoja baadaye.
Linda Thomas-Greenfield, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye amesema kuwa Marekani itachangia msaada wa kimataifa kwa kikosi cha polisi cha Kenya kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Balozi Linda ameongeza kuwa serikali ya Marekani tayari imeahidi kiasi cha dola za Kimarekani milioni 200 na itashirikiana na wadau ili kurejesha amani kabla ya uchaguzi mkuu ambao bado haujulikani utafanyika lini.
Hata hivyo, tangu wakati huo, suala hilo limekumbana na vizuizi vingi vya kisheria kwa upande mwingine, vita vya magenge vikiendelea kuongezeka na kukithiri katika mji mkuu wa Haiti na kwengineko.