Serikali ya Kenya imesema Alhamisi kwamba maafisa wake wa polisi hawatatumwa Haiti hadi masharti yote ya mafunzo na ufadhili yatakapotimizwa.
Kenya imejitolea kuongoza Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama nchini Haiti.
Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa idhini kwa Kenya kutuma ujumbe wa kimataifa wa kupambana na magenge ya kikatili katika nchi hiyo yenye matatizo ya Caribbean.
"Bajeti ya kutuma ujumbe Haiti ni dola milioni 600, kwa mwaka mmoja, kama Umoja wa Mataifa utafanya uamuzi," Kithure Kindiki Waziri wa Mambo ya Ndani aliiambia kamati ya bunge.
Waziri huyo ameiambia kamati ya bunge kuwa hakuna pesa za walipa kodi zitatumika kupeleka maafisa 1,000 wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kama sehemu ya Usaidizi wa Usalama wa Kitaifa nchini Haiti.
Anasema gharama ya kupelekwa kwao itagharamiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupitia michango ya hiari.
" Fedha hiyo inahusisha fedha kwa ajili ya kuandaa vikosi vya maafisa, kuwasafirisha kwenda, usafiri wao wakiwa huko Haiti, vifaa vyao vya mawasiliano, marupurupu yao na yote yanayoambatana na huduma yao, na baadaye fedha za kuwarudisha," Kindiki ameongezea.
Kindiki amesema Kenya haitapeleka maafisa hao 1000 wote kwa pamoja , watapelekwa kwa awamu tofauti.
Serikali inasema tayari imetumia dola za Marekani milioni 241 kuandaa baadhi ya maafisa wa polisi waliotengwa kwa ajili ya kutumwa Haiti.
Uamuzi wa serikali kutuma wanajeshi hao umezua utata nchini ikiwa watu wengine wanadai kuwa maafisa wa Kenya wanaweza kuwa hatarini kutokana na kukosekana kwa hali ya usalama nchini Haiti.
Wananchi wengine wamedai kuwa Haiti ni mbali sana na Kenya na labda ingekuwa bora ikiwa nchi jirani zingetuma vikosi vya usalama badala ya Kenya.
Mahakama Kuu ilikuwa imesitisha mipango ya kupelekwa kwa polisi Haiti, huku wakili aliyewasilisha kesi hiyo kudai kuwa hakukuwa na uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu hilo na kwamba Bunge lilikuwa likipuuzwa.
Baraza la mawaziri nchini Kenya limeidhinisha zoezi hilo na sasa suala hilo litapelekwa bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa.