Rais wa Uganda akifanya mazoezi Ikulu, nchini Uganda katika msimu wa Uviko19 / Picha: Reuters

Serikali ya Uganda imeamrisha wizara, na mashirika ya umma kuanzisha mazoezi ya kila wiki.

Serikali imesema ni kwa ajili ya kupunguza magonjwa yanayohusiana na hali ya maisha.

Mkuu wa huduma ya umma alisema haya katika barua ambayo aliandikia wizara za serikali.

"Hii ni kuwaarifu ....kutenga masaa mawili kila wiki katika taasisi zenu kwa jili ya kuhimiza afya njema," barua hiyo kutoka kwa Lucy Nayobe mkuu wa huduma ya umma ilisema, " Mchukulie suala hili kwa umakini."

Maagizo haya yalitolewa baada ya ripoti ya uchunguzi wa demografia na afya ya Uganda ambayo ilionyesha kuongezeka kwa unene kutoka asilimia 17 hadi 26 kati ya mwaka 2006 hadi 2022.

Uzito kupita kiasi na unene unahusishwa na hatari ya magonjwa ya kawaida kama vile ugonjwa wa kisukari, moyo na saratani.

Utafiti katika taasisi ya saratani ya Uganda umeonya katika ripoti ya mwaka 2022 kwamba changamoto ya saratani nchini Uganda inaweza kuongezeka kwa karibu asilimia 40 ifikapo 2030 kutokana na mabadiliko ya hatari na ukuaji wa idadi ya watu.

TRT Afrika