meno ya tembo kumi na moja yenye uzito wa kilo 32.924 yalikuwa yamefichwa kwa ustadi kwenye magunia ya nailoni/ Picha : DCI Kenya 

Polisi nchi Kenya kwa ushirikiano na maafisa wa kulinda wanyama pori KWS wamewakamata washukiwa wawili wakiwa na meno ya tembo.

Washukiwa hao, Paulo Telek na Paulo Kuya wote raia wa Tanzania, walitiwa nguvuni katika mtaa wa Majengo, kufuatia msako wa maafisa hao katika mtaa wa Majengo mjini Mombasa, pwani ya Kenya.

''Askari wetu waliofuatilia vidokezo waliwavamia Paul Kuya (36) na Paul Telek (29) katika maficho yao eneo la Majengo mjini Mtwapa ambapo walibaini meno ya tembo kumi na moja yenye uzito wa kilo 32.924 yakiwa yamefichwa kwa ustadi kwenye magunia ya nailoni ndani ya mifuko mitatu tofauti,'' ilisema taarifa ya Idara ya upelelezi DCI.

Kulingana na taarifa ya polisi, pembe hizo zenye uzani wa kilo 32.9, zinakadiriwa kuwa za thamani ya shilingi Milioni 3.3 za Kenya.

''Ilibainika kuwa wasafirishaji hao walikuwa wamesafiri kutoka Tanzania hadi Kenya kupitia mpaka wa Namanga, lengo lao lilikuwa kutafuta wanunuzi wa kununua bidhaa zao haramu,'' DCI iliendelea kusema.

Kwa sasa washukiwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mtwapa wakisubiri kufikishwa Mahakamani.

TRT Afrika