Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Uganda, Simon Byabakama amefichua kwamba raia ambao watatimiza miaka 18 baada ya tarehe 10 Februari 2025 hawatapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2026.
"Tunaamini ifikapo tarehe ya mwisho ya Februari 10, 2025, tutakuwa tumewasajili wananchi wote, mradi tu watatokea. Hata hivyo, Wananchi ambao watafikisha miaka 18 baada ya Februari 10, hadi siku ya kupiga kura mwezi Januari 2026, hao hawatakuwa sehemu ya daftari la kitaifa la wapiga kura,” alisema Byabakama.
Amesema hii ni kwa sababu Tume inahitaji muda wa kutosha kuandaa daftari la taifa la wapiga kura na kuamua idadi ya karatasi za kupigia kura kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026.
"Kuna Wananchi wa Uganda wanaofikisha miaka 18 kila siku na kwa wale ambao watakuwa na umri wa miaka 18 ifikapo tarehe 10 Februari 2025, wakati wa zoezi la uboreshaji watapewa fursa ya kujiandikisha kama wapiga kura," Byamukama alielezea Kamati ya Sheria na Masuala ya Bunge alipokuwa akiwasilisha Waraka wa Mfumo wa Bajeti wa 2025/26 wa Tume.
"Lakini kwa wale raia ambao watafikisha miaka 18 baada ya uboreshaji kumalizika hadi wakati wa kupiga kura, hatutaweza kuwajumuisha kwenye daftari la kitaifa la wapiga kura. Tarehe ya kikomo ya kujiandikisha ina maana, huu ni mwisho wa kuandikisha wapiga kura na pia kupokea maombi kwa wale wanaotaka kuhamishiwa kituo kingine,” alifafanua Byabakama.
Tume ya Uchaguzi inataka nyongeza ya Sh10.463Bn kwa ajili ya kuimarisha mishahara ya wafanyakazi ili kuwapa motisha na kuboresha utoaji wa huduma za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026.
"Ukiweka uandikishaji wa kura wazi, katika muktadha wa uchaguzi wa Uganda, unatengeneza kila aina ya porojo. Pili, unapangaje idadi ya karatasi kuchapishwa? Karatasi za kupigia kura hazichapishwi hapa nchini, zimechapishwa nje, unapangaje karatasi ngapi za kura utakazochapisha ikiwa huna idadi inayoweza kufahamika ya wapigakura katika wakati maalum?" Byabakama aliuliza kamati ya bunge.
Uchaguzi Mkuu Uganda
Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuanza kwa uboreshaji mkuu wa daftari la taifa la wapiga kura unaotarajiwa kufanyika kati ya tarehe 20 Januari 2025 hadi Februari 10, 2025.
Byabakama alilieleza Bunge kuwa wakati wa zoezi hili la uboreshaji, Tume inawalenga wananchi ambao wametimiza umri wa miaka 18 na walio zaidi ya miaka 18 lakini hawajawahi kujiandikisha kama wapiga kura.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Uchaguzi Mkuu wa 2026 umepangwa kufanyika kati ya Januari 12 na 9 Februari 2026 na Byabakama alitetea tarehe ya mwisho ya uandikishaji wapiga kura. Daftari la wapiga kura linatakiwa kuwa tayari ifikapo Septemba 2025 wakati uteuzi wa viti vya ubunge utakapofanyika.