Maabara ya Taifa ya Viwango nchini Uganda. Picha na UNBS

Mtandao wa Kupambana na Bidhaa Bandia, umefichua kuwa kufuatia mashauriano ya Muswada wa Sheria ya Kupambana na Bidhaa na Huduma Bandia, 2023, wananchi wengi wanatetea uwepo wa adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia ya kuzalisha bidhaa ghushi.

Hii ni pamoja na adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela kwa watakaopatikana na hatia ya kuzalisha bidhaa bandia.

Wito huu wa kuchukua hatua kali zaidi unatokana na wasiwasi kwamba baadhi ya bidhaa hizo zina hatari kubwa kiafya, na hivyo kusababisha mapendekezo ya kuongeza adhabu iliyopendekezwa ya kifungo cha miaka 10 jela.

"Adhabu iliyopendekezwa ni kifungo jela cha miaka 10, ambapo adhabu za awali zilikuwa miaka 2 au faini ya dola 545 (UGX milioni 2) . Wakati wa mashauriano, wengi walisema kuwa bidhaa ghushi ni hatari, na hivyo kusababisha kifo. Lengo la sheria ni kuonyesha hatari ya kujihusisha na bidhaa ghushi, hivyo kuweka adhabu kali,” Fred Muwema Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Bidhaa Bandia alisema.

Alitetea Muswada huo kwa kuangazia kuenea kwa dawa zisizo na viwango, zikiwemo dawa za malaria na za virusi vya Ukimwi, ambazo huchangia vifo vya waafrika kati ya 500,000 hadi milioni 1 kila mwaka.

“Tunapoteza maisha hata sasa, mtoto anakufa kwa malaria, pengine kutokana na madawa duni au ghushi ya kupambana na malaria. Hii haiathiri afya tu bali pia ina athari kubwa za kiuchumi," Muwema alielezea.

"Ikiwa mtoto ni mgonjwa, mama yake hawezi kufanya kazi, na kusababisha hasara ya kiuchumi ya dola za Marekani milioni 40 barani Afrika. Nchini Uganda, asilimia 20 hadi 30 ya bajeti yetu ya kitaifa inapotea kwa bidhaa ghushi, na hivyo kudhihirisha athari kubwa ya suala hili,” Muwema alieleza.

Wataalamu wa afya wanadai kuwa licha ya hatari kubwa zinazoletwa na bidhaa ghushi, suala hili mara nyingi halipati uangalizi wa kutosha kutokana na kukosekana kwa utafiti wa athari zake kiafya na kiuchumi.

"Muswada unafafanua wazi bidhaa ghushi, ambayo ni muhimu kwa vile Uganda imekuwa nchi pekee isiyo na sheria maalumu kushughulikia suala hili. Bidhaa bandia huiga bidhaa asilia. Pia kutakuwa na kampeni ya kuelimisha umma pindi sheria hiyo itakapopitishwa, ambayo inalenga kuelimisha wananchi jinsi ya kutambua bidhaa ghushi na kuhimiza kujidhibiti ili kuzuia kuenea kwao,” Muwema alisema.

TRT Afrika