Wabunge katika Kamati ya Kilimo nchini Uganda wameibua wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa kiwango cha sumu kuvu yaani aflatoxin katika chakula kinachozalishwa kote Uganda.
Wabunge wametoa mifano ya watu walioathiriwa kiafya.
Agnes Kirabo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Haki za Chakula alilitaka Bunge kuongeza juhudi katika kutekeleza Mpango wa Kudhibiti sumu kuvu Uganda. Alisisitiza kwamba uchafuzi wa chakula unaongezeka, ukichochewa na athari zisizotabirika za mabadiliko ya hali ya hewa.
"Tulitathmini sumu kuvu na kugundua kuwa viwango vinasalia kuwa vya juu, na vinaongezeka kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa," Kirabo alielezea.
“Wakulima hawawezi tena kutabiri ni lini mvua itanyesha, hali inayofanya ukaushaji na uhifadhi wa nafaka kuwa mgumu. Hii imechangia uchafuzi wa sumu kuvu, hasa katika mazao kama mahindi na mtama,” ameongezea.
Ripoti ya pamoja ya Kamati za Bunge za Kilimo na Afya Uganda, iliyochapishwa Aprili 2024, ilikadiria kuwa Uganda inapoteza dola milioni 38 kila mwaka katika mauzo ya nje kutokana na uchafuzi sumu kuvu.
Licha ya takwimu hii ya kutisha, suala hilo linaendelea.
Jennifer Driwaru, Mbunge wa Maracha, alifichua kuwa wabunge kadhaa wanakabiliana na changanmoto hiyo moja kwa moja. Aliripoti kuwa hivi karibuni wilaya yake ilipoteza watu watatu ndani ya wiki moja kutokana na matatizo yanayohusiana na ini.
"Tulimzika kijana wa miaka 19 jana, na leo tunazika watu wawili zaidi. Ini linashindwa; ni ugonjwa wa 'cirrhosis'. Katika siku mbili tu, tumepoteza watu watatu kwa hali hizi," Driwaru aliwaambia wabunge wenzake.
Nchini Uganda, sumu kuvu inachangia pakubwa ugonjwa wa ini.
Kulingana na Taasisi ya Saratani ya Uganda, kituo hicho hupokea wagonjwa wapya 170-200 wa saratani ya ini kila mwaka.
Kati ya 48-56 ya wagonjwa hawa wanahusishwa moja kwa moja na sumu kuvu.
Bunge linasema kutibu wagonjwa hawa hugharimu nchi takriban shilingi bilioni 3.12 (zaidi ya dola 841,000) kwa mwaka.