"Wanaume hawalii", ni kauli ya kawaida inayosikika barani Afrika. Na mara nyingi husikika wakati mwanamume anatakiwa kusonga mbele na kujikaza kiume! Hata wakati wa nyakati ngumu na mapambano makubwa zaidi.
Nchini Tanzania, mtu mmoja kati ya kila watu 20,000 wamejiua kutokana na matatizo ya afya ya akili kama vile msongo wa mawazo, mfadhaiko, hasira na matumizi ya dawa za kulevya katika miaka mitano iliyopita.
Mwili wenye afya, akili yenye afya! Hii ni kanuni ambayo sote tunaweza kuiishi! Ni muhimu kwamba kila sehemu ya mwili wetu iwe na afya na inafanya kazi, lakini kama ambavyo miili yetu inaweza kuugua, vilevile hata akili nazo huugua.
Michael Baruti ndiye mwanzilishi, mtayarishaji na mtangazaji wa ‘Men, Men, Men’ ambalo ni jukwaa mtandaoni kutoka Tanzania linayojadili afya ya akili ya Wanaume.
Mtangazaji wa zamani wa redio, Baruti aliona jukwaa hilo kuwa mahali pa kufanya kazi yake kwa sababu linatoa uhuru kwa urefu wa mada, gharama na uwezo wa kubadilishana mawazo. Lakini je, ina maana aliamka tu siku moja na kuamua hii ndiyo njia yake ya maisha ya baadae?
Changamoto za maisha kazini, madeni, ndoa na kushindwa shuleni kulichangia yote.
Siku za mwanzo
Katika mitihani yake ya kitaifa ya shule ya A level, Baruti hakufanya vizuri, jambo ambalo halikumpendeza baba yake. Kufeli kwake ni jambo ambalo lilimsababisha Michael alie.
“Wanaume hawalii”
Haya ni maneno aliyoyasema baba yake. Kukatishwa tamaa kuliongezeka na kulizidishwa na ukweli kwamba alitaka kuwa kijana mzuri shuleni, jambo ambalo hakulifanikisha, kwani alifeli katika hilo.
“Mwanangu sitakuwa hapa siku zote kukuongoza. Katika maisha, unafanya maamuzi, na utalazimika kuyaishi hayo maamuzi yako. Hivyo unaweza kuchagua kufanya vizuri zaidi au kuendelea kushindwa. Michael, sijawahi kukatishwa tamaa kama sasa; Nilitarajia mengi zaidi kutoka kwako.” Baruti anakariri maneno ya baba tangu ujana ambayo yalimfanya atokwe na machozi. Wakati huo baba yake alimwambia maneno hayo makali ...
Miaka kadhaa baadaye, baba yake alipata ugonjwa wa moyo. Mama yake aliacha kazi yake ili kumtunza miaka michache kabla ya hapo. Anakumbuka jinsi wakati mmoja wa safari zake za kawaida za matibabu, baba yake alikuja Dar es Salaam na kuuliza kama angeweza kulala nyumbani kwake.
“Nilikuwa na wasiwasi kuhusu mahali angelala na atakula nini. Nilikuwa sijiamini na nilihofia angeniona kuwa nimeshindwa!
Lakini kila kitu kilienda sawa, na upesi nikagundua kwamba alifurahi kuona tu mahali nilipoishi. Kuanzia wakati huo na kuendelea, nilihisi nimefanikiwa.”
Changamoto za maisha ziliendelea kuongezeka
Mwaka 2011, baba yake Baruti alifariki, na kwa muda mrefu, hakupenda kuzungumzia juu ya matarajio yote ambayo yalisababisha hisia zake za sonona.
Miaka mitatu baadaye, aliamua kuoa na kuanzisha familia. Huku deni la kifedha likiongezeka, mtoto mchanga njiani na kazi ikiwa katika hali ngumu. Bomu lilikuwa karibu kulipuka.
Alitafuta mtu wa kuzungumza naye jioni moja baada ya siku ngumu sana ya kazi…
Baada ya kutoa yote ya moyoni, aligundua kuwa alikuwa “mtu anayependa kufurahisha wengine" tena "bila mipaka". Hivyo ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya kuanza kupata faraja kupitia ushauri nasaha.
Hilo lilibadilika, na akaanza kuzungumza waziwazi kuhusu changamoto za afya ya akili alizokabiliana nazo na jinsi alivyoweza kupona baada ya kufunguka, kuzungumza na kuelezea mapito yake.
"Niliongea na kuongea, nililia na kuhisi kutua mzigo. Kwa muda mrefu, nilikuwa nikiweka kila kitu moyoni, nikiacha maisha yangu yajiendeshe popote pale. Sikuwahi kuzungumza au kushirikisha mtu yeyote mapito yangu. Kwa kweli, nilikuwa nikijificha mbali na kila mtu; Nilihisi nitalipuka. Nilijisikia vizuri zaidi baada ya kuzungumza na mtaalamu.”
Baada ya kufanya hivi, Baruti amekuwa akijifunza zaidi na zaidi kuhusu 'afya ya akili' na umuhimu wa kuzungumza na mtu. Anasisitiza umuhimu wa kufungua moyo na mawazo kwa mtaalamu ikiwa mambo yanasumbua.
Men. Men. Men, the podcast
Kila kitu kilianza kupitia chapisho moja tu kwenye ukurasa wa Twitter.
“Kuzungumza kuhusu matatizo yangu kuliokoa maisha yangu! Kulinifanya kushughulika na maisha yangu tena na nikaanza kuzungumza na watu wangu wa karibu kwa uwazi zaidi na kwa moyo mnyoofu.”
Baruti aliunda jukwaa hili ili wanaume kama yeye wanaopitia mambo magumu kama waweze kuzungumza na kuelezea hisia zao. Ni mahali ambapo wanaweza kuwa wazi na kujikubali wenyewe na wengine huku wakitambua si rahisi kuwa mwanaume.
"Tuna matarajio mengi ya kimaisha na tunatakiwa kujitengenezea mahali petu. Yote haya yanatokana na mila zetu na majukumu ya kijamii. Mambo kama hayo yanahitaji kujadiliwa, na pia yanapaswa kubadilika kadiri nyakati zinavyobadilika.”
African Podfest, kampuni ya kuwainua na kuwatia moyo watengeneza maudhui ya podikasti wa Kiafrika, ina utafiti unaoonyesha kuwa maudhui ya aina hio yanakua kwa kasi sana katika bara la Afrika, huku ukuaji wa haraka ukitoka Nigeria, Kenya na Afrika Kusini.
Kwa sasa jukwaa hilo linajivunia wingi wa wageni, kuanzia watu wenye mahitaji maalum, wanahabari na wanamichezo na hata aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania.
Pamoja na mada mbalimbali kama sonona, uzalishaji, tabia hatarishi, uwajibikaji, kujiamini, majukumu ya uzazi na kijamii.
"Tunawaalika wanaume kuwa wazungumzaji wageni na kuzungumza kuhusu masuala ya wanaume na matatizo yao.” Baruti anaieleza TRT Afrika, programu hiyo pia inajumuisha mwanasaikolojia wakati wa kurekodi ambaye anajibu maswali na kugusia masuala mbalimbali.
Baruti pia huandaa mikutano na warsha ili kuchimba zaidi maudhui na huwa na ‘vikundi vya majadiliano’ jijini Dar es Salaam na wanaume wengine kila baada ya miezi minne.
Vikundi na warsha zimeundwa kwa makusudi ili kuruhusu wanaume, kama Baruti, kukaa na kujadili masuala ambayo yanahusiana zaidi nao na yanaweza kuruhusu majadiliano ya wazi na kusaidia kuunda majadiliano yanayofuata katika programu hiyo.
"Binafsi, nimejifunza mengi kuhusu mimi mwenyewe kupitia podcast hii; inafurahisha sana kuelewa kwamba hauko peke yako; wanaume wengine wengi sana wanapitia uzoefu wa aina hiyo hiyo. Tunahitajiana, na hatimaye, tunaweza kusaidiana. Dhamira yangu kuwatia moyo watu wazungumze waziwazi!”
Podikasti hutoka kila baada ya wiki mbili kwenye tovuti maarufu za maudhui ya sauti.