Dkt Stergomena Tax, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hadi sasa hakuna Mtanzania anayeishi Sudan ambaye ameathiriwa na vita hivyo.
Mapigano makali yanaendelea Khartoum kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la wanamgambo, Rapid Support Forces (RSF), juu ya udhibiti wa Khartoum, na idadi ya waliouawa imefikia 185 na zaidi ya 1000 kujeruhiwa kulingana na Takwimu za Umoja wa Mataifa kuanzia Jumatatu.
Lakini idadi halisi ya waathiriwa inadhaniwa kuwa kubwa zaidi huku wengi waliojeruhiwa wakishindwa kufika hospitali, ambazo zenyewe zinapigwa makombora, kulingana na muungano rasmi wa madaktari.
Kati ya hospitali kuu 59 mjini Khartoum, takriban 39 kwa sasa "hazina huduma", ulisema umoja huo ambao uliripoti "uhaba mkubwa" katika vituo vilivyosalia.
Mapigano hayo pia yamesababisha uharibifu wa mali. "Serikali imeendelea kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na Ubalozi wetu uliopo Khartoum, ili kujua hali ilivyo.
Hali halisi ya wananchi wa Afrika Mashariki
Takriban Watanzania 210 wanaishi Sudan, kati yao 171 ni wanafunzi na wengine ni maafisa wa ubalozi na raia wengine,” Dkt Tax aliliambia Bunge mjini Dodoma jana.
Aliongeza: “Hadi sasa, hakuna Mtanzania ambaye ameripotiwa kuathiriwa na mapigano hayo. Serikali ya Tanzania inachukua hatua stahiki kwa ushirikiano na nchi jirani, jumuiya za kikanda, Umoja wa Afrika, na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kuwa Watanzania nchini na raia wengine wanakuwa salama.”
Katika taarifa ya Katibu Mkuu wa Idara ya watu wanaoishi ughaibuni, Roseline Njogu, kuna takriban Wakenya 3000 wanaoishi na kufanya kazi nchini Sudan na hadi sasa hakuna majeruhi yalioripotiwa. Idara hii ya serikali inafuatilia hali inayoendelea kwa wakati huu kwa karibu sana.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia inawataka raia nchini Sudan kujiandikisha kwa ajili ya ufuatiliaji wa usalama huku kukiwa na wasiwasi wa kiusalama.
Wabunge wa Sudan Kusini wanatoa wito kwa viongozi kuzingatia hatua ya haraka ya kuwahamisha raia wa Sudan Kusini waliokwama nchini Sudan kutokana na ghasia zinazoendelea Khartoum na miji mingine mikubwa.
Hadi sasa, serikali bado haijatoa taarifa zozote kuhusu usalama wa Wasudan Kusini nchini Sudan.