Wanajeshi wazuia makao makuu ya upinzani nchini Uganda kabla ya maandamano

Wanajeshi wazuia makao makuu ya upinzani nchini Uganda kabla ya maandamano

Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliwaonya wanaotaka kuandamana nchini humo kuwa wanachezea moto
Bobi Wine  alisema chama chake hakikuwa kikiandaa maandamano ya Jumanne, lakini kinaunga mkono./ Picha: Reuters 

Wanajeshi na polisi walifunga makao makuu ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda siku ya Jumatatu katika kile ambacho msemaji wa polisi alikitaja kuwa ni hatua ya tahadhari kabla ya maandamano ya kuipinga serikali yaliyopangwa kufanyika Jumanne licha ya kupigwa marufuku.

Katika machapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X, mkuu wa chama cha National Unity Platform Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, alisema maafisa wa usalama wamezingira makao makuu ya NUP katika mji mkuu Kampala, wakizuia mtu yeyote kuingia au kutoka.

Wine alisema viongozi kadhaa wa NUP "wamekamatwa kwa vurugu" na pia alionyesha picha za wanajeshi kwenye majengo hayo pamoja na malori ya jeshi yaliyokuwa yameegeshwa.

“Jeshi na polisi wamevamia na kuzingira ofisi za Jukwaa la Umoja wa Kitaifa...” alisema. "Utawala waoga unaogopa sana watu kwa sababu wanajua ni kiasi gani wamewadhulumu!" aliongeza Wine.

Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke hakujibu mara moja alipotafutwa ili kutoa maoni yake kuhusu kukamatwa kwa watu hao.

Wine, 42, nyota wa pop aliyegeuka mwanasiasa, katika miaka ya hivi karibuni ameibuka kuwa mpinzani mkubwa kwa Rais mkongwe Yoweri Museveni, 79, ambaye ameongoza taifa hilo la Afrika Mashariki tangu 1986.

Vijana wa Uganda ambao wameongoza maandamano ya hivi majuzi wanapanga kuandamana hadi bungeni siku ya Jumanne wakikaidi marufuku ya maandamano hayo, ambayo yananuiwa kukemea madai ya ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya utawala wa muda mrefu wa Museveni.

Wine alisema chama chake hakikuwa kikiandaa maandamano ya Jumanne, lakini kinaunga mkono.

Msemaji wa polisi Rusoke alisema vikosi vya usalama vimechukua hatua za tahadhari dhidi ya kile alichokiita NUP "uhamasishaji wa maandamano". "Tumekuwa tukifuatilia (hili). Shughuli zao ziliinua bendera nyekundu na tulichukua hatua za tahadhari," alisema.

Shutuma za upinzani na wanaharakati

Maandamano ni halali kikatiba nchini Uganda lakini waandalizi lazima wapate vibali mapema kutoka kwa polisi, ambavyo ni nadra sana kutolewa.

Viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za serikali umeenea nchini Uganda na kwa muda mrefu wamekuwa wakimshutumu Museveni kwa kushindwa kuwashtaki maafisa wa ngazi za juu wafisadi ambao ni watiifu kisiasa au wanaohusiana naye.

'Mnachezea moto'

Hata hivyo maandamano haya yanakuja wakati Rais Yoweri Museveni ametoa onyo kali kwa yeyote atakayeshiriki kuwa atakuwa anacheza na moto, akiashiria kuwa anajihatarishia maisha yake mwenyewe.

Museveni aliwaonya vijana wanaopanga maandamano mtandaoni wasichochewe na nguvu za nje kuvuruga amani ya taifa.

Maandamano haya yanahusishwa na maandamano yanayoendelea Kenya yanayoongozwa na vijana wanaolalamikia ufisadi serikalini na utawala mbaya na hali ngumu ya maisha.

Wimbi la maandamano

Vijana kutoka nchi kadhaa za Afrika wamekuw awakielezea katika mitandao ya kijamii kuwa wanataka kuiga mfano wa voijana wa Gen Z wa Kenya wanaopinga serikali ya William Ruto katika mfululizo wa maandamano yanayoingia mwezi mzima sasa.

Kumekuwa na wito wakufanyika maandamano ya vijana nchini Nigeria kuanzia Agosti Mosi, japo pia mamlaka zimepiga marufuku dhidi yake.

TRT Afrika na mashirika ya habari