Chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda kimeanza kuchunguzwa baada ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Akol kugundua kuwa zaidi ya wanafunzi 400 wa Shahada ya Uzamili walishindwa kumaliza masomo yao kwa wakati uliotarajiwa.
Bunge la Uganda limepata ushahidi unaoonyesha kuwa kwa wastani, wanafunzi walichukua zaidi ya miaka minne ya masomo kukamilisha utafiti wa shahada ya uzamili ilhali muda ulioidhinishwa kwa mafunzo ya chuo kikuu ni miaka 2.
Wakati huo huo chuo kingine kinachofahamika kama Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Makerere pia kimewekwa kwenye uangalizi baada ya wanafunzi 322 wa Shahada ya Uzamili kugunduliwa kuwa wamechukua wastani wa zaidi ya miaka 4 ya masomo kukamilisha utafiti wa masomo hayo.
Hii ni zaidi ya muda ulioidhinishwa wa chuo kikuu kwa programu za uzamili za miaka 2.
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Akol amebainisha kuwa kati ya wanafunzi 3,044 waliojiandikisha kwa ajili ya masomo mbalimbali ya uzamili katika kipindi cha miaka kumi (mwaka wa masomo 2013/14 hadi 2020/2021), wanafunzi 1,931 walihitimu na kuacha wanafunzi 1,113 ambao bado hawajahitimu.
Zaidi ya hayo, Akol ameliambia bunge pia kati ya wanafunzi 190 waliojiandiakisha kwa Programu za Uzamivu kwa kipindi cha miaka 10 (mwaka wa masomo 2013/14 hadi 2020/2021) ni wanafunzi 60 tu ndio waliohitimu. Wanafunzi 130 bado hawajahitimu.
Amesema baadhi ya ucheleweshaji huo ulichangiwa na ucheleweshaji wa usimamizi na changamoto zinazohusiana na wanafunzi kama vile uhaba wa fedha.