Umoja wa Mataifa, UN, inasema wakimbizi kutoka nchi jirani za uganda wanedlea kukimbilia nchi hiyo.
" Uganda inashuhudia kuongezeka kwa idadi ya wananchi wa Sudan wanaowasili. Zaidi ya watu 33,000, ikiwa kati yao 19,000 wamewasili Kampala tangu kuanza kwa 2024, ili kutafuta usalama kutoka kwa vita ambavyo vimeendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja," shirika la wakimbizi la UNHCR limesema katika taarifa.
Wasudan wengi waliofika wanatoka Khartoum, na wengi wana elimu ya kiwango cha chuo kikuu.
UNHCR inasema Uganda ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi barani Afrika, ikiwa na takriban watu milioni 1.7 hasa kutoka Sudan Kusini na DRC. Hata hivyo ipo miongoni mwa operesheni 13 za juu zaidi za UNHCR ambazo hazikufadhiliwa kikamilifu duniani mwaka 2023.
" Takriban watu 2,500 wanawasili Uganda kila wiki, hasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini, wakilzaimishwa kuhama na migogoro inayoendelea na changamoto zinazohusiana na hali ya hewa," imeongezea.
" Ongezeko la mara kwa mara la wakimbizi haliangazii vichwa vya habari lakini pamoja na upungufu wa fedha, kunaweka shinikizo kubwa katika huduma za ulinzi na usaidizi zinazotolewa kwa wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi, hivyo kuhatarisha mfumo thabiti wa ulinzi wa Uganda na modeli ya kukabiliana na wakimbizi," UNHCR imesema.
Mnamo mwaka wa 2024, mpango wa kuhudumia wakimbizi wa nchini Uganda unahitaji dola milioni 858 kwa washirika 96 kusaidia zaidi ya wakimbizi milioni 1.67 na wanajamii wenyeji milioni 2.7, Hata hivyo asilimia 13 tu ya fedha zinazohitajika zimepokelewa.
Kutokana na mapungufu ya ufadhili, sekta ya afya, ambayo inahudumia wakimbizi na wakazi tayari imeathirika sana. UN inasema Idadi ya wafanyikazi wa vituo vya afya imelazimika kupunguzwa na hakuna vifaa vya kutosha kukidhi mahitaji muhimu ya kiafya.