Wakili wa Kiongozi wa Kikundi cha Lord's Resistance Army, LRA Uganda Joseph Kony siku ya Alhamisi aliiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuahirisha kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Kony akidai mteja wake hayupo, hivyo kuna hatari ya kupoteza "muda na pesa."
Kony, 62, amekuwa akisakwa na Mahakama ya ICC yenye makao yake mjini The Hague tangu mwaka 2005 kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia utawala wa miongo mitatu wa ugaidi na kundi lake la waasi la Lord's Resistance Army (LRA) katika mataifa kadhaa ya Afrika.
Mahakama ya ICC ilitangaza miezi mitano iliyopita itafanya vikao mwezi Oktoba kuthibitisha makosa 36 dhidi ya Kony, ambaye kwa sasa hajulikani aliko.
Wakili wa Kony aliyeteuliwa na Mahakama Peter Haynes aliwaomba majaji kabla ya kesi hiyo "kuacha kesi hiyo hadi wakati ambapo Bw Kony atakapofika mbele ya mahakama" ana kwa ana.
Ombi jipya
Haynes, katika hati ya mahakama, alisema alikubaliana na waendesha mashtaka wa ICC ambao mwaka 2015 walisema kusikilizwa bila kuwepo kwa Kony "kunaweza kuwa na gharama kubwa ya muda, pesa, juhudi bila manufaa yoyote."
Mnamo Machi, majaji wa ICC walikubali ombi jipya la mwendesha mashtaka mkuu Karim Khan la kutaka kesi za uthibitisho zianze bila kuwepo kwa Kony.
Haynes pia alitoa sababu nyengine kwa nini kesi inapaswa kuahirishwa. Alidai kisheria kusikilizwa kwa kesi ya mtu asiyekuwepo mahakamani kunaweza tu kufanywa iwapo tu mshukiwa aliwahi kufika mahakamani awali.
Haijulikani ikiwa Kony yuko hai
"Kwa vile bwana Kony hajawahi kufika mbele ya mahakama, kesi hiyo ikiwa hayupo hairuhusiwi kisheria chini ya Mkataba wa ICC," Haynes alisema kwenye taarifa.
"Haikujulikana pia kama Kony yuko hai huku kukiwa na "ripoti nyingi za umma" zinazoonyesha kuwa amefariki. Hata kama Kony hatimaye atapatikana, anapaswa kuhukumiwa katika mahakama ya ndani ya nchi yake," Haynes alisema.
Mahakama ya Kampala mapema mwezi huu ilimpata na hatia kamanda mwingine wa zamani wa LRA, mfano wa "uwezo wa mahakama za Uganda kuendesha kesi za kimataifa," Haynes alisema.
Thomas Kwoyelo alipatikana na hatia kwa makosa 44 yakiwemo mauaji, ubakaji, utesaji, wizi na utekaji nyara kwa nafasi yake katika harakati za waasi.
Aliyekuwa kijana wa madhabahu Kony alianzisha LRA katika miaka ya 1980 kwa lengo la kuanzisha utawala unaozingatia Amri Kumi.
Kundi hilo lilianzisha uasi dhidi ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambao ulienea hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan. Iliua zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 ambao walilazimishwa kuwa watumwa wa ngono, askari na wapagazi.