Rachael Kabue anafuga paka katika kituo chake cha Feline Sanctuary Nairobi / Picha:  TRT Afrika

Pendekezo jipya la "ushuru wa paka" limezua malalamiko kwa wapenzi wa paka jijini Nairobi, nchini Kenya.

Kama sehemu ya Rasimu ya Mswada wa Kudhibiti Ustawi wa Wanyama, Kaunti ya Nairobi inataka wamiliki wote kusajili paka wao na kulipa ada ya kila mwaka ya leseni ya shilingi 200 za Kenya ($1.50).

Pia watalazimika kuhakikisha wanawapiga chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa angalau mara moja kwa mwaka. Miongoni mwa masharti hayo pia ni kuhakikisha wanyama wao "hawana kelele itakayovuruga" amani ya wengine, na kuwazuia paka ambao wanakaribia kupata uja uzito.

Madhumuni ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, kulingana na maafisa wa Kaunti, ni kukuza umiliki unaowajibika wa wanyama wanaofugwa na kusaidia kudumisha hifadhi data ya kina ya wamiliki wa paka na utekelezaji wa chanjo na viwango vya afya.

Wanasema hatua hiyo pia itashughulikia suala la paka waliopotea ambao wanaweza kupatikana popote katika mji mkuu wa Kenya.

"Mlezi wa paka"

Wamiliki wa paka wamekuwa na majibu makali, hasa wale wanaoona ushuru huo kama mzigo kwa wamiliki.

"Nina paka watatu. Hiyo ni shilingi 600 za Kenya (karibu $5) kwa mwaka. Hiyo si sawa,” alisema Yasmin Amina, mmiliki wa paka wa muda mrefu.

Kaunti ya Nairobi inataka wamiliki wote kusajili paka wao na kulipa ada ya kila mwaka ya shilingi 200 za Kenya ($1.50) / Picha TRT Afrika

"Ni kanuni yake. Kwa nini paka wanatengwa? Je, wanachangia kidogo katika jamii yetu kuliko mbwa?" Rachael Kabue, anayejulikana kwa upendo kama "mlezi wa paka" wa Nairobi.

Kabue mwenye nyumba ya vyumba vinne na zaidi ya paka 600, wengi wao wakiwa wamepotea njia aliowachukua kutoka mitaani.

Nyumba yake imegeuzwa kuwa kituo cha kutunza familia yake ya paka bila kuchoka, akihakikisha wanalishwa, kupewa chanjo na kuoshwa kwa upendo. Kwa Kabue, kodi iliyopendekezwa ni jambo ambalo "lingeharibu familia yake."

'Haijafafanuliwa wazi'

“Unaweza kufikiria ingegharimu kiasi gani? … Hii ni njia nyengine tu kwa serikali kuchukua fursa ya watu wanaojaribu kufanya mema … Paka hawa ni familia yangu. Ni wakati wa kuwapigania," aliiambia Anadolu.

"Badala ya kututoza ushuru, serikali inapaswa kusaidia watu kama mimi ambao wanasaidia kupunguza idadi ya paka wanaozurura. Wanapaswa kuhimiza kuasili na kutoa rasilimali, na sio kuifanya iwe ngumu kwetu," anaongezea.

Naomi Mutua, mtetezi wa dhati wa ustawi wa paka, alihudhuria mkutano wa hivi majuzi wa umma kuhusu mswada huo uliofanyika katika Kaunti ya Jiji la Nairobi.

"Kwa wazi ilionekana kuwa mambo yote hayakuwa na mpangilio," Mutua, ambaye anaendesha ukurasa wa Facebook wenye zaidi ya wafuatiliaji 25,000 wa paka, aliambia Anadolu.

“Nyaraka zilizotolewa kwenye mkutano huo zilikuwa tofauti na zile zinazopatikana mtandaoni, na kusababisha mkanganyiko. Maneno yaliyotumika katika mswada huo, kama vile ‘maafisa walioidhinishwa’ na ‘ustawi,’ hayakuelezwa waziwazi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwetu kuelewa kinachotarajiwa kutoka kwetu kama wamiliki wa paka.

Alisema maafisa, walipoulizwa kuhusu malengo ya muswada huo, "hawakuweza kutoa ufafanuzi."

"Hilo linatufanya tuwe na mashaka zaidi kuhusu kile wanachojaribu kufanya," alisema Mutua, anayejiita "mama wa paka" wa Nairobi. Pia alionyesha kukosekana kwa uwazi katika mchakato huo, haswa "mashirika ya kitaalamu ambayo yanadaiwa kutoshirikishwa wakati wa kuanda mswada."

Utapiamlo wa paka

Chama cha Kenya cha Kulinda na Kutunza Wanyama, mojawapo ya sauti zinazoongoza kwa ustawi wa wanyama nchini Kenya, pia kimeelezea wasiwasi wake kuhusu pendekezo hilo.

Licha ya kazi yake kubwa katika uwanja huo, Shirika hilo lilithibitisha katika taarifa kwamba "hawajashauriwa kama washikadau katika kuandaa mswada huu."

Mjadala kuhusu ushuru wa paka pia umeleta masuala makubwa zaidi ya uwajibikaji kwa jamii na jukumu la umiliki wa wanyama katika maeneo ya mijini.

Mitaa ya Nairobi ni makazi ya maelfu ya paka waliopotea, wengi wao wanakabiliwa na utapiamlo, magonjwa na kutelekezwa.

Athari ya ushuru

"Idadi ya paka wanaopotea katika jiji imekuwa ikiongezeka na hiyo inasababisha masuala zaidi ya afya ya umma na kuenea kwa magonjwa," alisema.

Alidokeza kuwa fedha zinazotokana na ushuru wa paka zinatakiwa kusaidia mipango ya ustawi wa wanyama, ikiwa ni pamoja na huduma za kuhasi kwa paka.

"Pesa hizo zitaenda moja kwa moja kusaidia wanyama wengine," aliiambia Anadolu.

"Ikiwa utaiangalia kwa njia hiyo, ushuru huu unaweza kuwa na athari chanya."

Hata hivyo, wengine wana wasiwasi kwamba ushuru unaweza kuwa na athari tofauti na kusababisha ongezeko la paka walioachwa, wakisema kuwa mswada huo unaweka mzigo usiofaa kwa wamiliki wa wanyama bila kushughulikia sababu kuu za shida ya kupotea.

Tatizo halisi “si paka walio na nyumba, bali wale ambao hawana,” alisema Benedita Achieng, mfugaji mwengine wa paka.

TRT Afrika