Uhalifu wa kivita ambao ni pamoja na mateso, adhabu ya viboko, utekaji nyara na vitendo vya kigaidi vinaweza kushitakiwa katika Mahakama ya ICC. / Picha: Wengine 

Katika mitandao ya kijamii, Wakenya wanaendesha kampeni maalumu huku wakihimizana kujaza fomu ya mahakama ya Kimataifa ya jinai, ICC, kwa ajili ya kuishitaki serikali ya Rais William Ruto.

"Chini ya Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (“OTP”) inaweza kuchambua taarifa kuhusu uhalifu unaodaiwa ndani ya mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, mauaji ya halaiki na uchokozi), iliyowasilishwa kwake. kutoka kwa chanzo chochote," fomu hiyo inasema.

Kampeni hii inakuja huku kukiwa na matukio ya utekaji nchini Kenya. Wiki iliyopita, vijana saba waliotekwa Disemba 2024 waliachiliwa.

Je, nini kinahitajika kumshitaki mtu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inazingatia malalamiko kadhaa:

Uhalifu wa kivita ambao ni pamoja na mateso, utekaji, adhabu ya viboko na vitendo vya kigaidi vinaweza kushitakiwa katika Mahakama ya ICC.

Makosa ya jinai ikiwa ni kesi inayojumuisha vitendo vyote vinavyofanywa kwa nia ya kuharibu kikundi cha kitaifa, kabila au dini.

Uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwa ni vitendo vinavyofanywa kama sehemu ya shambulio lililoenea au la kimfumo dhidi ya raia wowote, kama vile mauaji, kuhamisha watu kutoka makazi yao, mateso na ubakaji.

Nani anaweza kushtaki?

Mahakama ya Kimataifa ya ICC inaweza kusikiliza kesi ya mtu ikiwa nchi ambapo kosa lilifanyika ni mwanachama wa ICC au ikiwa nchi ya asili ya mhalifu ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda ICC.

Kesi inaweza kuletwa ICC na nchi yoyote mwanachama wa mkataba wa Roma, bila kujali uhusika wowote katika kosa linalodaiwa. Mwendesha Mashtaka wa ICC na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wanaweza kuwasilisha kesi mbele ya ICC.

Baadaye Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC (OTP) hufanya uchunguzi kwa kukusanya ushahidi, kuhoji watu wanaochunguzwa na kuhoji waathiriwa na mashahidi, kwa madhumuni ya kupata ushahidi wa kutokuwa na hatia au hatia ya mtuhumiwa.

Nchi zenye kesi mbele ya ICC

Kesi inayohusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ilianza Juni 2004. Inahusisha madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa katika muktadha wa vita vya kijeshi nchini DRC tangu tarehe 1 Julai 2002.

Kuanzia 1 Januari 2022 uchunguzi unalenga Mashariki mwa DRC, katika Mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini,

Machi 2005 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwasilisha kesi kuhusu tuhuma za mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanyika huko Darfur, Sudan, tangu tarehe 1 Julai 2002.

Januari 2004 kesi dhidi ya kikundi cha waasi wa Lord's Resistance Army (LRA) ililetwa mbele ya mahakama kwa uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu

Nchi nyingine zenye kesi katika mahakama ya ICC ni Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Burundi miongoni mwa mataifa mengine.

TRT Afrika