Rekodi zinaonesha ongezeko la wahamiaji haramu kutoka kusini mwa jangwa la Sahara, wakiwa katika harakati za kutafuta maisha mazuri katika nchi za 'Mashariki ya Kati' / Picha: AA     

Watu 16 wanahofiwa kupoteza maisha na wengine 16 hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji haramu kuzama katika eneo la pwani ya Djibouti, Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa limesema siku ya Jumanne.

Ajali hiyo imetokea wiki mbili baada ya chombo kingine kilichokuwa kimebeba wahamiaji wengi kutoka Ethiopia ilipozama katika pwani ya Djibouti, katika harakati zao za kupata maisha bora ughaibuni.

"Ni janga kubwa sana, boti imezama nchini Djibouti ikiwa na wahamiaji 77 wakiwemo watoto," Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema kwenye chapisho kwenye ukurasa wake wa X, zamani ukijulikana kama Twitter.

"Watu 28 bado hawajulikani walipo, 16 wamekufa," lilisema shirika hilo huku likisema kuwa litaongeza nguvu katika juhudi za uokoaji."

Watoto ni kati ya waathirika

Yvonne Ndege, msemaji wa shirika hilo, aliiambia AFP kwamba watu 16 waliofariki ni pamoja na watoto na mtoto mchanga, bila kutoa maelezo zaidi.

Balozi wa Ethiopia nchini Djibouti, Berhanu Tsegaye, alisema kwenye ukurasa wake wa X kwamba boti hiyo ilikuwa imebeba wahamiaji wa Ethiopia kuelekea Yemen na kwamba ajali hiyo ilitokea Jumatatu usiku karibu na Godoria kaskazini mashariki mwa Djibouti.

Boti nyingine iliyokuwa imebeba zaidi ya watu 60 ilizama katika pwani ya Godoria mnamo Aprili 8, kulingana na IOM na ubalozi wa Ethiopia nchini Djibouti.

Kuelekea Saudi Arabia

IOM ilisema wakati huo miili ya wahamiaji 38, wakiwemo watoto, ilipatikana, huku watu wengine sita wakitoweka.

Ubalozi wa Ethiopia ulikuwa umesema kuwa boti ilikuwa imebeba wahamiaji wa Ethiopia kutoka Djibouti kuelekea Yemen.

Kila mwaka, makumi ya maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika wanajasiria "Njia ya Mashariki" kuvuka Bahari Nyekundu na kupitia Yemen ili kujaribu kufika Saudi Arabia, kutoroka migogoro au maafa ya asili, au kutafuta fursa bora za kiuchumi.

"Wakati wa safari zao, wengi wanakabiliwa na hatari za kutishia maisha ikiwa ni pamoja na njaa, hatari za kiafya na unyonyaji mikononi mwa wasafirishaji haramu wa binadamu na wahalifu wengine," IOM ilisema katika taarifa yake Februari.

Ongezeko la Wahamiaji

Ndege alisema takwimu za IOM kutoka 2023 zilionyesha kuwa "idadi ya watu wanaojaribu kuvuka inaongezeka."

Kulingana na IOM, Waethiopia wanachangia asilimia 79 ya wahamiaji 100,000 waliowasili Yemen mwaka jana kutoka Djibouti au Somalia, waliosalia wakiwa Wasomali.

Ethiopia, ambayo ndio nchi ya pili kwa idadi ya watu barani Afrika, imekumbwa na migogoro wakati baadhi ya maeneo yake yakipitia hali ngumu ya ukame.

Zaidi ya asilimia 15 ya raia wake milioni 129 wanategemea misaada ya chakula.

Mwezi Februari, IOM ilisema kuwa kwa mujibu wa Mradi wake wa Wahamiaji Waliopotea, takriban watu 698, wakiwemo wanawake na watoto, walikufa wakivuka Ghuba ya Aden kutoka Djibouti kwenda Yemen mwaka jana.

TRT Afrika