Wagombea watatu wanaowania kitia cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika wanakutana 13 Disemba 2024 katika mjadala katika makao makuu ya Tume ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 2025, na marais na viongozi wa nchi za Afrika, eneo la Mashariki linastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume, huku eneo la Kaskazini likistahili kugombea nafasi ya Naibu Mwenyekiti.
Raila Odinga kutoka Kenya, Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madacar wanagombea kiti hicho cha uongozi wa kibara.
Katika mjadala huu watatarajiwa kutetea sera zao za kibara na kuwashawishi waafrika kuwa wana uwezo wa kuongoza Tume hiyo ya Umoja wa Afrika.
Mjadala wa kwanza 2017
Mnamo mwaka wa 2017, Mjadala wa kwanza kabisa wa Umoja wa Afrika uliopewa jina la Mjadala Afrika ulifanyika kama jukwaa la wagombea waliojitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa AUC ili kuwahutubia wananchi wa Afrika katika mazingira ambayo yalihimiza mazungumzo na kuelewa nafasi na wajibu wake.
Mdahalo huo uliwapa wagombea nafasi ya kueleza maono yao ya jinsi watakavyoongoza mabadiliko ya Afrika kupitia utekelezaji wa Mamlaka ya AU na Ajenda ya Afrika ya 2063.
Mdahalo huo pia uliwapa fursa wananchi wa Afrika na wadau wengine kuuliza maswali kwa wagombea kuhusu masuala wanayoyataka kushughulikiwa ili kukuza bara na kuhakikisha Afrika inafikia malengo yake ya maendeleo jumuishi na endelevu na kuwa mdau mkuu katika uwanja wa kimataifa.
Kuendeleza mjadala
Novemba 2018, marais wa Afrika walipitisha uamuzi wa kuimarisha uwazi na uhalali wa uteuzi wa uongozi wa Tume ya AU na kufanya mjadala wa wagombea wote ni kati ya mikakati ya kufanya hivyo.
Marais wakati huo waliamua kuwa wagombea wote wa nafasi ya Mwenyekiti wa Tume watashiriki katika mjadala wa kutetea sera zao ambao utaonyeshwa moja kwa moja kwa raia wa Afrika kupitia vyombo vya habari.
Watatarajiwa katika mdahalo huo kuwasilisha maono na mawazo yao kuhusu utekelezaji wa Ajenda ya maendelao ya bara maarufu kama Agenda 2063.
Mdahalo utaendeshwa kwa lugha ya Kifaransa na Kiingereza, na tafsiri ya wakati mmoja itatolewa kwa wagombea na watazamaji katika lugha zote sita za kazi za Umoja wa Afrika yaani Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kihispania, na Kiswahili.
Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat kutoka Jamhuri ya Chad, alichaguliwa tena kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa muhula mwengine wa miaka minne kuanzia 2021-2024 katika uchaguzi uliofanyika tarehe 6 Februari 2021.
Wakati huo ambapo kulikuwa na mlipuko wa Uviko 19, hakuna nchi iliyoonyesha nia ya kutaka nafasi ya Faki.