Kituo cha mpaka wa Namanga kwa upande wa Kenya./Picha: Wengine   

Wajumbe wa kamati ya huduma za jamii ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameazimia kuzifanyia kazi changamoto za kibiashara katika eneo la Namanga.

Akizungumza kutoka eneo hilo linalotenganisha nchi ya Tanzania na Kenya, mmoja wa wajumbe hao, Kanini Kega amesema atalipeleka suala hilo katika mikutano ya bunge la EALA kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo zinazowakabili wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili.

"Tutachakata na kuwasilisha hoja hizo kwa wabunge wenzetu, nia ni kuona tunavuka mipaka yetu bila vizuizi vyovyote," alisema mjumbe huyo kutoka Kenya.

Kulingana na mjumbe wa huyo wa EALA, changamoto za kibiashara zinazoshuhudiwa katika mpaka huo zimesababisha upotevu mkubwa wa pesa na kuharibika kwa bidhaa za chakula.

Moja ya tatizo sugu, kulingana na wafanyabiashara mpakani Namanga, ni upatikanaji wa Hati za Dharura za Kusafiria (ETD) kwa upande wa Tanzania, ambayo ikishatolewa, hutumika kwa safari moja tu, hivyo kumlazimu msafiri au mfanyabiashara kuomba nyingine, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Biashara za ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) ilikua kwa asilimia 11.2 na kufikia dola bilioni 10.91 kwa mwaka 2022, kutoka dola bilioni 9.81 mwaka 2021.

Katika salamu zake za mwaka mpya, Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki alitanabaisha kuwa jumuiya hiyo imejizatiti kuongeza kiwango chake cha ufanyaji biashara ya ndani hadi kufikia asilimia 40.

TRT Afrika