Uganda inasafirisha nje kahawa, pamba na mali ghafi nyengine kupeleka nchini Marekani chini ya mpango wa biashara wa AGOA. Picha: Reuters

Wabunge kutoka maeneo yanayolima kahawa Uganda wamepinga vikali kukomeshwa kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Kahawa Uganda, UCDA na majukumu yake kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo.

Wabunge hao wanadai kuwa hatua kama hiyo itauwa zao la kahawa kama ilivyouwa zao la vanilla na chai ambazo ziliwekwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Kilimo.

Joseph Ssewungu mbunge wa Kalungu Magharibi alihoji kwa nini Serikali inapinga wananchi wa eneo la Buganda kuwa matajiri, “Kupitia UCDA, watu wameanza kulima kahawa, UCDA imewasaidia. Kwa nini mnaogopa watu kuwa matajiri? Kwa nini? Kwa nini mnaogopa watu kuwa na pesa?" aliuliza katika mjadala bungeni.

Connie Nakayenze mbunge wa Mbale alishangazwa na Kamati ya Bunge ya Kilimo kutoa picha nzuri ya mafanikio ya UCDA, na baadae kugeuka na kupendekeza kuunganishwa kwa UCDA.

Nakayenze amesema UCDA ikiwekwa chini ya Wizara ya Kilimo itakuwa sawa na kunyonya damu watu wa mkoa wa Buhisu walio mashariki mwa nchi.

"Ripoti ilieleza wazi jukumu la UCDA ambalo ni pamoja na kutimiza viwango vya soko, pia ilisema UCDA hutoa bei elekezi kwa wakati kila siku...Katika eneo letu la Bugisu ukiondoa UCDA ni sawa na kumwaga damu ya Bagisu wote kwa sababu wanategemea kahawa,” alisema Nakayenze.

Aisha Kabanda mbunge wa Butambala aliongezea, “Siyo kwamba serikali iwe na fursa ya kuwanyang’anya watu kila kitu wanachoanzisha wanavyotaka. Unapounda vyombo sio vya kwako, ni vya wananchi. Watu wakisema ndio umevitengeza na sisi tunataka, sio juu yako kuviondoa, unavyotaka,” aliiambia serikali.

Serikali yatetea kauli yake

Bright Rwamirama, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ufugaji alisema kuwa mjadala wa wabunge wengi ulifanywa kwa mitazamo isiyoeleweka.

Amesema kuna sababu ya serikali kutoa muda wa mpito wa miaka mitatu kufafanua kwa kina umuhimu wa mamlaka ya kahawa kuvunjwa.

"Nyingi ya hoja hazitokani na maamuzi sahihi juu ya nia ya Serikali. Kuhusu uhalali wa miaka mitatu hii,... Serikali iliamua kuruhusu kipindi cha mpito cha miaka mitatu, ili kuhakikisha kuwa kero za wadau zinashughulikiwa ili tusonge mbele pamoja," Rwamirama aliliambia bunge.

Jitihada za baadhi ya Wabunge za kusimamisha kusomwa kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Kahawa, 2024 kwa mara ya pili zilipotea baada ya Wabunge 159 kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kupitishwa kwa Muswada huo kwa Kamati, dhidi ya Wabunge 77 waliotaka Muswada huo uondolewe.

Kuzingatiwa kwa Muswada huo kutaendelea Bunge litakaporejea, ingawa haijajulikana lini itakuwa hivyo, kwa sababu Spika wa Bunge aliahirisha Bunge.

TRT Afrika