Kiongozi wa upinzani Ousman Sokno aliondolewa makosa ya ubakaji lakini anasem amashtaka haya yanalenga kumzuia kuwania urais | Picha AA

Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) kwa pamoja zimeshutumu vikali ghasia zilizozuka Ijumaa nchini Senegal baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kupewa kifungo cha miaka miwili kwa kosa la ‘kupotosha vijana’.

Mitandao ya kijamii na ya kutuma ujumbe imefungwa nchini Senegal huku watu 9 wakiripotiwa kuuawa katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji kufuatia hukumu hiyo.

Sonko hakuwepo mahakamani wakati wa kutolewa kifungo hicho na hakimu ameagiza kuwa akamatwe punde akionekana. Wafuasi wake wanahofia kuwa kifungo hicho ni njama ya kumzuia kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Katika taarifa, mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alishutumu vikali ghasia hizo.

“Matendo kama haya yanachafua taswira ya demkorasia ya Senegal, ambayo kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikijivunia," alisema Faki, huku akiwahimiza viongozi wote wa kisiasa kutumia hekima na mashauriano kutatua zogo hili.

AU iliomba mamlaka nchini Senegal kuheshimu uhuru wa kufanya maandamano ya Amani.

Ecowas imeelezea kusikitishwa na vifo vilivyotokea na kutoa wito wa ustahamilivu katika kutafutia suluhisho tofauti zao kwa njia ya Amani.

“Ecowas inashutumu ghasia zilizolenga vikosi vya usalama, mali ya umma, mali za watu binafsi na kuvuruga amani,’’ iliongeza.

Huku hali ikionekana kuwa tete, vyombo vya habari vimeripoti kutumwa vikosi vya kulinda usalama katika mji mkuu Dakar, ambao walishika doria Ijumaa, katika barabara za mji.

Katika medani ya uhuru, mjni Dakar, mita chache kutoka kasri la rais, polisi waliondolewa na badala yake jeshi lilishika doria kuhakikisha usalama.

Msemaji wa serikali Abdou Karim Fofana alihakikishia taifa kuwa hali imeimarika.

Ecowas imeongeza kuwa tume yake inafuatilia kwa makini mambo yanavyoendelea nchini Senegal na kuwahimiza ‘‘kila mmoja kutetea sifa nzuri ya nchi hiyo ya kuwa na Amani na uthabiti.’’

Sonko alifunguliwa mashtaka ya ubakaji na kutoa vitisho vya kumuua Adji Sarr, mfanyakazi wa saluni ya urembo mjini Dakar mnamo 2021.

Mahakama limuondolea Sonko makosa ya ubakaji Alhamisi, lakini ikampa kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kupotosha vijana, na hivyo kumnyima fursa ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwakani.

Sonko alikuwa wa tatu katika uchaguzi uliopita 2019 nyuma ya rais Macky Sall, lakini wakati wa kusikilizwa kesi, alidai kuwa mashtaka hayo yanalenga kumhujumu asiweze kuwania urais 2024.

TRT Afrika