Rais wa Ghana Nana Akufo Akufo-Addo ameiomba Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS kushughulikia suala la viongozi kubadilisha katiba za nchi zao ili kujirahisishia kukaa madarakani kwa muda mrefu.
Akufo-Addo anasema vitendo kama hivyo vinachochea hasira katika jamii na "kuunda misingi yenye kuchochea visingizio vya jeshi kuingilia utawala kwa misingi ya kurekebisha."
Kiongozi huyo wa Ghana alizungumza siku ya Ijumaa katika mji wa Winneba, kusini mwa Ghana, ambako bunge la ECOWAS linafanya kikao chake.
Wabunge wa ECOWAS wamekutana chini ya kaulimbiu "Changamoto zinazohusiana na mageuzi kinyume na katiba ya mipaka ya Muda wa Serikali na Urais katika Afrika Magharibi - Wajibu wa Bunge la ECOWAS."
Akufo-Addo anasema majadiliano ya kina kuhusu ukomo wa mihula ya urais yatahakikisha kwamba wananchi "hawakati tamaa" kuhusu demokrasia.
Majaribio yaliyoshindikana
Alitoa wito kwa viongozi wanaotumia "migogoro ya kisheria" "kubadilisha kanuni za kikatiba na kutishia taasisi za umma kwa lengo moja la kubaki madarakani."
Matamshi ya Akufo-Addo yanakuja baada ya viongozi kadhaa, ndani ya ECOWAS na nje ya jumuiya hiyo, kubadilisha katiba za nchi zao ili kuwaruhusu kuchaguliwa tena bila vikwazo vya kisheria.
Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda na Equatorial Guinea ni baadhi ya nchi ambazo viongozi wake walibadilisha katiba ili kuwaruhusu kuchaguliwa tena.
Hapo awali wakuu wa nchi za ECOWAS walikuwa wamejaribu kuwawajibisha marais kutumikia mihula miwili pekee, lakini pendekezo hilo halikupitishwa kamwe. Majaribio matatu kama haya yalishindikana, pamoja na moja mnamo 2015.
Moja ya majukumu muhimu ya bunge la ECOWAS ni "kukuza na kutetea kanuni za haki za binadamu, demokrasia, utawala wa sheria, uwazi, uwajibikaji na utawala bora," amesema Addo.
Bunge la ECOWAS lina wabunge 115 kutoka mataifa 15 wanachama.