Mkutano wa ECOWAS / Picha: AP

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika magharibi (ECOWAS) imeandaa kikao maalum katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Jumapili Desemba 10.

Ofisi ya Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara imesema katika taarifa baada ya mazungumzo na wakuu wa muungano wa ECOWAS.

Viongozi wa Afrika magharibi watafanya mkutano huo wa kilele baadaye mwezi huu huku eneo hilo likijitahidi kukabiliana na msururu wa mapinduzi na kuzuia migogoro ya jihadi katika Sahel.

Viongozi hao walikutana mara ya mwisho mwezi Agosti kujadili hali ya Niger baada ya mapinduzi ya Julai 26 ambayo yalimpindua Rais aliyechaguliwa Mohamed Bazoum, ambaye tangu wakati huo amezuiliwa katika makazi yake huko Niamey.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ina wanachama 15 wakiwemo Benin, Burkina Faso, Cabo Verde, Cote D'ivoire, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Liberia, Mali, Niger, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, na Togo.

Hata hivyo, tangu 2020, wanachama wake wanne; Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea kati ya nchi wanachama hao 15, wameshuhudia mabadiliko ya uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Hata hivyo, tangu wakati huo, wote wamesimamishwa kutoka jumuiya hiyo, na hawatawakilishwa katika mkutano wa kilele wa Abuja.

Aidha, jaribio jingine la mapinduzi lilifanyika jumapili nchini Sierra Leone, mwanachama mwingine wa ECOWAS na kusababisha vifo vya watu 21, kulingana na maafisa wakuu nchini humo.

Mikakati ya mkutano huo inajiri huku rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo akisema kuwa ghasia mbaya zilizoshuhudiwa wiki hii, zinazohusisha wanajeshi wa walinzi wa taifa ni "jaribio la mapinduzi" wakati jeshi lilipowaamuru warudi kwenye kambi.

Mgogoro kati ya askari wa walinzi wa kitaifa na vikosi maalum vya walinzi wa rais Alhamisi usiku, katika mji mkuu wa Bissau, ulipelekea vifo vya watu wawili.

Rais Embalo, ambaye alikuwa Dubai kuhudhuria mkutano wa tabia nchi wa COP28, aliwasili Bissau Jumamosi na kusema "jaribio la mapinduzi" lilimzuia kurudi nchini humo.

ECOWAS ilisema "tunalaani vikali vurugu na majaribio yote ya kuvuruga utaratibu wa kikatiba na utawala wa sheria nchini Guinea-Bissau".

"ECOWAS pia inataka kukamatwa na kushtakiwa kwa wahusika wa tukio hilo kwa mujibu wa sheria," Jumuiya hiyo yenye makao yake makuu Abuja, iliongeza katika taarifa yake Jumamosi.

Jumuiya hiyo ya kikanda pia lilionyesha "mshikamano kamili na watu na mamlaka za kikatiba za Guinea-Bissau".

AFP