Balozi wa Ufaransa nchini Niger alisafirishwa nje ya nchi mapema Jumatano asubuhi, shirika la habari la Reuters linaripoti kunukuu vyanzo viwili vya usalama.
Hatua hii inakuja takriban mwezi mmoja baada ya serikali ya kijeshi kutangaza kufukuzwa kwake.
Utawala wa kijeshi ambao ulichukua mamlaka katika mapinduzi ya Julai ulimuamuru balozi wa Ufaransa Sylvain Itte kuondoka nchini ndani ya saa 48 mwishoni mwa Agosti kujibu kile walichokiita vitendo vya Ufaransa "kinyume na maslahi ya Niger".
Lakini amri hiyo hapo awali ilipuuzwa na Ufaransa, ambayo imekataa kuwatambua viongozi wa mapinduzi, na kusababisha maandamano ya kila siku mbele ya ubalozi wa Ufaransa.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema mwezi huu kwamba Itte na wafanyakazi wake walikuwa wakishikiliwa mateka katika ubalozi huo.
Mwishoni mwa wiki, Macron alisema balozi huyo alikuwa katika harakati za kutolewa na atarejea Ufaransa. Pia alitangaza kuwaondoa wanajeshi 1,500 wa Ufaransa wlaioko nchini humo.