DRC : Daktari Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani 2018 kugombea Urais

DRC : Daktari Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani 2018 kugombea Urais

Daktari huyo aliyepata umaarufu kwa kuwatibu kinamama hadi kubatizwa jina la 'Baba anayewatengeneza Kinamama'
Wagombea wengine wanayo nafasi ya kufikisha faili zao kwenye Tume ya Uchaguzi CENI kabla ya tarehe 8 mwezi huu wa Octoba ili kushiriki uchaguzi mkuu/ Picha Reuters 

Na Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Kinshasa, DRC

Daktari Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Nobel 2018 ametangaza jumatatu hii mjini Kinshassa kwamba atakuwa mgombea wa uchaguzi wa Urais baadae tarehe 20 Disemba mwaka huu.

Daktari Denis Mukwege alitangaza uamzi huo kwenye mkutano na vyombo vya habari mjini Kinshasa.

Ameamua kuingia kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais katika hatua za mwisho kabisa na kuwasilisha faili zake kwenye Tume huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI).

''Siwezi kusubiria hadi mwaka wa 2028, Sijachukua uamuzi huu kwa sababu ya maslahi au kwa sababu ya kutaka madaraka. Lakini kwa lengo la kuokoa taifa langu. Kesho itakuwa nimechelewa. Nakwenda sasa kujitupa kwenye uchaguzi.'' Alisema Dkt Mukwege.

Uamzi huo wa Dkt. Mukwege hata hivyo ulikuwa unasubiriwa kwa miezi kadhaa. Jina lake lilikuwa linazungumzwa sana miongoni mwa watu wanaoweza kuwa wagombea wa uchaguzi. Na wiki za hivi karibuni hali iliashiria hivyo.

Watu ambao walikuwa wanasititiza wakimtaka awe mgombea wanaamini kwamba huu ndio wakati muafaka na uamzi sahihi.

''Inabidi kuwa na moyo wa kuachana na matakwa au raha za kibinafsi na kufikiria kwanza uzalendo,'' aliongeza Dkt Mukwege.

Dkt Mukwege pia alizindua azimio lake ambalo limetungwa kwa nguzo kumi na mbili, ikiwemo amani, usalama na ulinzi sambamba na kupambana dhidi ya hisia za ubaguzi nchini, na haki na sheria sawa kwa wote pamoja na utawala wa sheria.

Azimio lake linaonekana kwenda sambamba na vita ambavyo Dk Mukwege amekuwa anapigania kwa muda mrefu na hasa kutokana na kutowajibikia viongozi walioko madhila wanayopata raia.

Alianza hotuba yake akiomba ukimya wa dakika moja ili kuwakumbuka waathirika wote wa migogoro nchini DR Congo. '' Mimi ni mwananchi ambae nimehuzunishwa saana, mimi ni mwanamageuzi''. Alitangaza Bwana Mukwege '' Hatuko pamoja na raia, tumejiweka kwenye ubinafsi.''

Aidha Bwana Mukwege alikemea vikali '' Wimbi za ahadi hewa zilizofanywa na watawala wasiowajibika. Na hii imenifanya kuchukua maamuzi.''

Oroodha ya wagombea Urais

Daktari huyo aliyepata umaarufu kwa kuwatibu kinamama hadi kubatizwa jina la 'Baba anayetengeneza Kinamama'

''Nchi yangu iko hatarini. Hali ni tete Mashariki mwa Nchi yetu kukiwa na vikosi vya kigeni, Rasli mali zetu zinaporwa , dhiki ya maisha ni kubwa kwa raia, ndio maana nimeamua mara hii kugombea urais ili kumaliza changamoto hizo,'' alisema Dkt Mukwege.

Dk Mukwege anakuja kuongeza orodha ya watetezi kwenye uchaguzi huo wa urais.

Mwishoni mwa juma , Rais Felix Tchisekedi alitangaza kuwa atawania tena urais na kuongoza Muungano mkubwa wa Vyama vilivyo karibu na Serikali'' Union Sacree''.

Wakati huo huo Mpinzani Mkuu Martin Fayulu naye pia alibainisha uamzi wake wa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Wagombea wengine wanayo nafasi ya kufikisha faili zao kwenye Tume ya Uchaguzi CENI kabla ya tarehe 8 mwezi huu wa Octoba ili kushiriki uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 20 Disemba 2023.

TRT Afrika