Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizitaka nchi kote ulimwenguni kukomesha mizozo ya kivita kama sehemu ya makubaliano ya Olimpiki, huku Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ikitarajiwa kufunguliwa baadaye Ijumaa.
Guterres alikutana na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach na kusema kuwa Michezo hiyo ni fursa ya amani.
"Nataka kueleza uungaji mkono kamili wa Umoja wa Mataifa kwa IOC," Guterres alisema. “Tunaishi katika ulimwengu uliogawanyika ambapo mizozo inaongezeka kwa njia kubwa.
"Mateso ya kutisha huko Gaza, vita vinavyoonekana kutokuwa na mwisho nchini Ukraine, mateso mabaya kutoka Sudan hadi DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), kutoka Sahel hadi Myanmar.
"Amani kwa ajili ya Olimpiki"
"Katika wakati kama huu ni muhimu kusema kwamba mpango wa kwanza kurekodiwa, katika historia, wa amani halisi ulikuwa usitishaji wa Olimpiki."
Wakati wa Michezo ya Olimpiki katika Ugiriki ya kale migogoro yote ilikoma kwa muda wa Michezo ili kuruhusu mashindano kuendelea.
"Katika wakati ambapo Michezo ya Olimpiki itaanza ni wakati wa kukumbusha ulimwengu umuhimu wa usitishaji wa Olimpiki na kuufanya ulimwengu kuelewa kwamba lazima tunyamazishe bunduki," aliongeza.
Michezo hiyo itaanza baadaye Ijumaa na kumalizika Agosti 11 kwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 10,500 wanaowakilisha mataifa na maeneo 206.
Wanariadha wasio na upande wowote
Hizi ni pamoja na timu ya Palestina, ambayo ingawa si mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, ina Kamati rasmi ya kitaifa ya Olimpiki, pamoja na wanariadha kutoka Urusi na Belarus, ambao watashindana kama wasio na upande wowote bila bendera au nembo kufuatia uvamizi wa Ukraine mwaka 2022.
"Kwa hivyo huu ndio wakati ambapo ombi langu kubwa ni kwa nchi kuja pamoja na ari sawa kama wanariadha watakavyokuja pamoja wakati wa Michezo ya Olimpiki huko Paris," Guterres alisema.