Takriban watu 115 wameokolewa kutoka mikononi mwa wapiganaji waasi wa kundi la ADF huko Irumu, kaskazini Mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Uokoaji huo ulifanywa katika oparesheni ya pamoja ya jeshi la taifa la FARDC na kikosi cha jeshi la Uganda (UPDF) dhidi ya ngome za waasi hao katika eneo la chifu la Walese Vonkutu Kaskazini Mashariki mwa DRC.
"Mateka mia moja na kumi na tano waliokuwa wakishikiliwa na waasi wa ADF waliachiliwa Ijumaa Septemba 15 kutoka mikononi mwa watekaji nyara huko Ndalya, kijiji kilichoko kilomita 50 kutoka kituo cha kibiashara cha Komanda kwenye barabara ya kitaifa nambari 4 katika wilaya ya Irumu (Ituri)", alisema Christophe Munyanderu, mratibu wa shirika la haki za binadamu katika eneo la Irumu.
Kanali Mak Hazukay Mongba, msemaji wa operesheni za pamoja za FARDC-UPDF, alithibitisha habari hii na kwamba "matokeo ya ukombozi huu bado ni ya mapema".
Kanali Mak Hazukay, ambaye anaahidi kutoa maoni yake kuhusu suala hilo katika siku zijazo, anadokeza kuwa mapigano yanaendelea katika eneo hilo ili kuwaondoa waasi kutoka katika ngome zao.
Kwa mujibu wa shirika la haki nchini humo, (CRDH), ambalo linafanya kazi katika eneo la Irumu, majeshi hayo mawili yalianzisha mashambulizi ya kina katika msitu wa Ndalya Ijumaa asubuhi. Lengo la operesheni hizi ni kuwatimua waasi hao ambao wanawaua raia na mara kwa mara kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya watu.
Pia makundi hayo yamekuwa yakilaumiwa kushambulia na kuchoma moto magari, haswa kwenye barabara ya Komanda-Luna.
Mateka 115 walioachiliwa ni pamoja na wanawake 29 na watoto 16, kulingana na chanzo hicho hicho, ambacho kiliongeza kuwa kundi la pili la mateka 21 wa zamani waliwasili Ndalya mapema Jumamosi asubuhi.
Ni baada ya hatua hii tu ndipo wanaweza kukabidhiwa kwa familia zao," anaelezea Christophe Munyaderu, mratibu wa NGO katika eneo la Irumu.
Anasema kuwa mateka hawa wa zamani wengi wao ni abiria ambao walinaswa katika mashambulizi ya kuvizia ya ADF kwenye barabara ya Komanda-Luna.