Askari wa FDLR) akitembea kuelekea kituo cha usambazaji karibu na Kambi ya Lushubere huko Masisi, kilomita (maili) kaskazini-magharibi mwa Goma, Desemba 19, 2008. / Picha Reuters Maktaba 

Na Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Mapigano makali yameripotiwa kuzuka Jumapili katika eneo la Masisi, Mashariki ya Demkrasia ya Congo moja mwa maeneo ya Mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

Mapigano hayo yamehusisha Waasi wa kikundi cha M23 dhidi ya Makundi yenye silaha watiifu kwa Serikali maarufu 'Wazalendo'.

Kwa upande mwingine, waasi wa M23 walikabiliana na vikosi vya serikali katika eneo la Kibumba, kwenye umbali wa kilomita 20 na mji wa Goma. Mapigano hayo yamesababisha kukatika kwa umeme Jumatatu jioni, sehemu kubwa ya mji mkuu huo wa Kivu ya Kaskazini ilikumbwa na ukataji wa umeme.

''Laini kubwa ya pili inayoleta umeme kutoka shirika la Virunga Energy iliharibiwa vibaya sana kwenye mapigano kati ya Waasi wa M23 na Jeshi la Congo'', ilifafanua taarifa ya Shirika hilo linalogawa umeme katika mji wa Goma.

Hii imesababisha athari mbaya sio tu kwa makaazi lakini pia kwa hospitali kwa muda usiojulikana hadi sasa, kwa vile ni vigumu mafundi kufika katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli za ukarabati.

Mapigano yamekuwa yanaarifiwa katika eneo hilo kwa zaidi ya wiki mbili bila kusimama.

Mmoja wa viongozi wa Mashirika ya Kiraia katika eneo la Masisi,Téléphore Vitomboke anahofia iwapo Waasi hao wataelekea upande wa eneo la Mushaki ,inawez kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya eneo hilo na mji wa Goma kama ilivyokuwa miezi kadhaa ya nyuma.

Eneo hilo la Mushaki ki msingi liko chini ya ulinzi wa vikosi vya Burundi katika mpango wa Vikosi vya kulinda amani vya Afrika Mashariki.

Lakini vikosi hivyo vya Burundi vimekuwa vinalaumiwa na Kikundi cha M23 tangu Jumatatu kwa madai kwamba vilishiriki kwenye mapambano ya hivi karibuni '' kwa kukiuka mkataba wa usitishwaji wa mapigano'' kulingana na makubaliano yaliosainiwa mijini Nairobi na Luanda mwezi Machi mwaka huu.

Hata hivyo Burundi imekana shutuma hizo.

Mapigano hayo yanaarifiwa wakati muhula wa Vikosi vya kulinda amani vya Jumuiya ya Afrika Mashariki EACRF unelekea kufikia ukingoni baadae mwezi ujao wa Disemba.

Serikali ya DRC ilitangaza kwamba haina imani tena na vikosi hivyo vya EAC kwa madai kwamba majeshi hayo yameshindwa kuwadhibiti waasi na kusimamisha vita huku Kinshassa ikijiandaa kupokea vikosi vya SADC Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini Mwa Afrika kudhibiti usalama katika eneo hilo la Mashariki mwa Congo.

Wakuu wa nchi za SADC walikutana Ijumamosi mjini Luanda kuandaa mkakati wa kutuma vikosi hivyo ingawa tarehe rasmi haikutangazwa.

TRT Afrika