Martin Fayulu (pichani) aligombea na kushindwa dhidi ya Rais Felix Tshisekedi katika uchaguzi wa Desemba 30, 2018 DRC. / Picha: AA

Wajumbe wa viongozi wakuu wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliwasili Afrika Kusini siku ya Jumatatu ili kujadiliana kuhusu kuratibu uchaguzi ujao katika nchi hiyo ya Afrika ya kati, maafisa walisema.

Rais Felix Tshisekedi, aliye madarakani, anawania muhula wa pili katika uchaguzi wa Desemba 20.

Wachambuzi wengi wanamwona rais huyo kuwa na uwezekano wa kushinda kura hiyo, ikizingatiwa kwamba upinzani wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umegawanyika kati ya wapinzani kadhaa.

Siku ya Jumatatu, wajumbe wanaowakilisha wanasiasa watano wakuu wa upinzani - ambao wote wanashiriki uchaguzi ujao - walifika katika mji mkuu wa utawala wa Afrika Kusini Pretoria kwa mazungumzo.

'Ugombea wa pamoja'

Walijumuisha wajumbe wa Moise Katumbi, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la zamani la Katanga; mgombea urais wa zamani Martin Fayulu; waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponya; Delly Sesanga, mbunge; na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2018 Denis Mukwege.

"Ugombea wa pamoja ungehitajika ili kuepuka kutawanya kura za upinzani," mshiriki mmoja wa mazungumzo hayo, ambaye alikataa kutajwa jina, alisema.

Lakini mshiriki mwingine, ambaye pia aliomba kutotajwa jina, alisema mazungumzo hayo yalilenga kutafuta “utaratibu wa pamoja wa kuepusha udanganyifu” katika uchaguzi huo.

"Hatukwepeki mjadala wa mgombea mmoja, lakini tunachohitaji zaidi ya yote ni ukweli kwenye sanduku la kura," alisema.

TRT Afrika