Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, wanafanya mkutano wao wa kawaida nchini Tanzania.
Kwa sasa, EAC inajumuisha nchi saba: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania.
Ajenda ya mkutano huo wa marais ni pamoja na kupokea ripoti ya majadiliano ya kuidhinishwa kwa shirikisho la Somalia katika EAC.
Mazungumzo ya Somalia kujiunga na EAC yalianza mwezi Agosti mwaka huu, huku kamati maalumu ya nchi za Afriak Mashariki ikifanya mazungumzo na Somalia kuhusu ombi lao.
Marais pia watajadiliana kuhusu maendeleo ya mchakato wa Nairobi unaoongozwa na EAC kuhusu kurejesha amani Mashariki mwa DRC.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilituma wanajeshi kwa mara ya kwanza katika eneo hilo lenye hali tete nchini DRC mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23.
Maeneo haya ya kaskazini mwa DRC ni maeneo yaliyoshuhudia mashambulizi kutoka kwa vikundi vyenye silaha, yanaendelea kutishia juhudi za amani na utulivu zilizopatikana hadi sasa.
Hata hivyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema vikosi vya Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) vitaondoka nchini kufikia tarehe 8 Disemba.
DRC imekataa kikosi hicho kuongeza muda zaidi ikidai wanajeshi wa Afrika Mashariki hawajaweza kutatua tatizo ya ukosefu wa usalama hasa lile la mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23.
DRC inasema ingependelea nchi za Afrika Kusini kutuma majeshi huko.
Mwezi Novemba marais wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, walikutana mjini Luanda nchini Angola, kuzungumzia hali ya usalama Mashariki mwa DRC.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukamilisha mpango wa kupeleka vikosi vya kijeshi hivi karibuni nchini DRC (SAMIDRC).
Marais katika mkutano wao pia watajadili maendeleo ya mbinu endelevu za ufadhili wa EAC na kufanya mashauriano ya katiba ya shirikisho la kisiasa la EAC.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir anatarajiwa kushika uenyekiti wa Jumuiya ya EAC kutoka kwa mwenzake wa Burundi rais Evariste Ndayishimiye ambaye muda wake wa uenyekiti umefikia ukomo.