Kwa mara ya kwanza katika historia yake, nafasi ya Katibu Mkuu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC) itashikiliwa na mwanamke, baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Peter Mathuki kuteuliwa kuiwakilisha Kenya nchini Urusi.
Caroline Mwende Mueke, anatarajia kumalizia kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa mtangulizi wake ambaye kwa sasa ataiwakilisha Kenya kama balozi, kufuatia mabadiliko yaliyotangazwa na Rais William Ruto hivi karibuni.
Kulingana na Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya hiyo, Rais wa nchi husika anaweza kupendekeza jina kwa nafasi ya Katibu Mkuu, kabla ya kuidhinishwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.
Nafasi hiyo huwa ni ya mzunguko kwa kila nchi mwanachama, na mteule huhudumu kwa muda wa miaka mitano.
Mueke ni nani?
Mueke, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya sera za umma, amepata fursa ya kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa, UNESCO, UNDP na ujumbe wa amani Sudan ya Kusini.
Hata hivyo, uteuzi wa Mueke utasubiria kuidhinishwa kwa mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki.
Matumizi mabaya ya ofisi
Uongozi wa Mathuki, ambaye amekuwa EAC toka mwaka 2021, ulighubikwa na madai ya matumizi mabaya ya fedha, hali iliyoweka rehani nafasi yake ya Ukatibu Mkuu.
“Sheria za matumizi ya fedha ndani ya Jumuiya zinataka uwazi katika matumizi ya kila fedha itokayo na iingiayo,” alisema Dennis Namara, mwenyekiti wa kamati ndogo ya fedha ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wakati wa ufunguzi wa kikao cha 5 cha bunge hilo, jijini Nairobi.
“Hakuna maelezo yoyote kuhusu zaidi ya dola milioni 6 zilizokusanywa na hata Katibu Mkuu mwenyewe ameshindwa kuzitolea maelezo hapo bungeni.”
Hata hivyo, katika taarifa yake ya ufafanuzi wa tuhuma dhidi ya Mathuki, Jumuiya hiyo imeishambulia makala iliyochapishwa kwenye gazeti mojawapo Afrika Mashariki.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa Machi 11, EAC imedai kuwa hakuna msingi wowote katika tuhuma hizo dhidi ya Mathuki na kwamba, zililenga tu kuchafua taswira ya Katibu Mkuu huyo wa zamani.
"Tumesikitishwa sana na kitendo cha jarida hilo kushindwa kumpa Mathuki wasaa wa kujibu tuhuma hizo kulingana na kanuni asili za haki kabla ya kuchapa makala hiyo," imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kulingana na EAC, Sekretarieti ya Jumuiya hiyo, huandaa ripoti maalumu ya ukaguzi kutoka nchi zote wanachama katika ukanda huo, kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi.
"Kwa kuwa Katibu Mkuu aliingia madarakani miaka 3 iliyopita, hakuna ripoti ya ukaguzi mbaya dhidi yake, na isitoshe taarifa hizi hupatikana katika ofisi ya Jumuiya," EAC imesema.
Kabla ya kuteuliwa kuingoza EAC, Mathuki aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EALA) na kabla ya hapo aliwahi pia kuwa mbunge ndani ya EALA.
Anakuwa Mkenya wa pili kushika nafasi ya Ukatibu Mkuu baada ya Francis Muthaura.