Wanajeshi wa jeshi la Uganda, sehemu ya wanajeshi wa EACRF, wanaporudi kambini kutoka katika doria huko Bunagana / Picha: Reuters

Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa habari baada ya mkutano na Baraza la Usalama wakati wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt Peter Mathuki alisema makubaliano hayo yatakamilishwa hivi karibuni baada ya Monusco kujiondoa rasmi kutoka DRC ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

"Dhahiri Umoja wa Usalama wa UN una hamu kubwa na unathamini jukumu la Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kusaidia usalama wa mashariki mwa DRC," alisema Dkt Mathuki kuongeza, "Wamekubaliana kuanzisha mfumo utakaosaidia vikosi vyetu nchini DRC, na walisema wanapofunga Monusco na kupunguza idadi yao nchini DRC, watapenda kuimarisha EACRF."

Dkt Mathuki alisema ameliomba Baraza la Usalama kuwa wanapojiandaa kupunguza Monusco, wanaweza kusaidia kufadhili EACRF ambayo kwa sasa ina zaidi ya wanajeshi 4,000 kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini.

"Tumependekeza kufadhili EACRF, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisema wanakutana mwezi Disemba ambapo tutaweza kujua kiasi gani wanaweza kupunguza kutoka Monusco na ni kiasi gani wataweza kupata kufadhili EACRF," alisema Dk. Mathuki.

Nchi saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana mwezi Aprili mwaka huu kuanzisha jeshi la kikanda ili kujaribu kumaliza vurugu na shughuli za waasi katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ghasia nchini Congo zimesababisha hali ya dharura za kibinadamu mbaya zaidi na kudumu kwa muda mrefu ulimwenguni, ambapo zaidi ya watu milioni 27 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na karibu watu milioni 5.5 wamelazimika kukimbia makazi yao, kulingana na ripoti za Umoja wa Mataifa.

"Misioni za kulinda amani zilizoanzishwa, kwa namna moja au nyingine kwa miaka 25, zimeshindwa kukabiliana na uasi na migogoro ya silaha inayoisambaratisha Jamhuri."

Rais wa DRC Felix Tshisekedi

Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatano kwamba kuondolewa kwa Monusco ni muhimu kwa kumaliza mzozo kati ya wananchi wa Congo na ujumbe huo.

"Kuendeleza kasi ya kuondolewa kwa Monusco kunakuwa ni jambo la lazima kwa kuepusha mivutano kati ya ujumbe huo na wananchi wetu," alisema.

"Misioni za kulinda amani zilizoanzishwa, kwa namna moja au nyingine kwa miaka 25, zimeshindwa kukabiliana na uasi na migogoro ya silaha inayoisambaratisha Jamhuri."

Mwaka 2010, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinachojulikana kama Monusco kilichukua nafasi ya operesheni ya awali iliyoitwa Monuc, ambayo ilianzishwa mwaka 1999 kusaidia kuleta amani na utulivu DRC.

Lakini licha ya mabilioni ya dola kutumika kwa moja ya vikosi vya kulinda amani vikubwa zaidi vya Umoja wa Mataifa, zaidi ya makundi ya waasi 120 bado yanafanya shughuli zao katika sehemu kubwa za Mashariki mwa Congo karibu miaka miwili baada ya kumalizika rasmi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

TRT Afrika na mashirika ya habari