Hali ya utulivu inaonekana katika jiji la Kinshasa wakati zikisalia saa chake kuelekea uchaguzi mkuu. 

Juma Issihaka

TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania

Joto la uchaguzi mkuu katika taifa la Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, linaendelea kupanda, huku Watanzania wakisisitiza umuhimu wa amani ili kulinda uhusiano wa kibiashara na kindugu baina ya wananchi wa mataifa hayo.

Watalaamu wa masula ya uchumi na baadhi ya raia wa Congo waliopo nchini Tanzania, wanauangalia uchaguzi huo kuwa ndio utakaoamua ama kuimarisha au kuzorotesha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo jirani na wananchi wake wanaohusiana kwa miongo kadhaa.

Uhusiano kibiashara

Uchaguzi huo, unafanyika katika kipindi ambacho mauzo ya Tanzania nchini DR Congo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 18 katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Ongezeko hilo ni kutoka dola za Marekani milioni 7.53 mwaka 1997 hadi kufikia dola za Marekani milioni 280.54 mwaka 2022, kwa mujibu wa takwimu za kanzidata ya Shirika la Umoja wa Mataifa la COMTRADE.

Sambamba na hilo, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), zinabainisha taifa la DR Congo limewekeza miradi 19 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 463.34 nchini Tanzania.

Ingawa mataifa hayo yanapakana, pia raia wake wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili. Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania ni wazungumzaji wa Kiswahili. Upande wa DR Congo inakadiriwa asilimia 40 ni wazungumzaji wa lugha hiyo hasa waliopo katika Mikoa ya Mashariki mwa nchi hiyo.

Uhusiano wa mataifa hayo umekwenda mbali zaidi mwezi Septemba mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilipotangaza kuondoa viza kwa raia wote wanaotoka Congo DR.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa nchini Tanzania ya mwaka 2020, DR Congo, ndiyo nchi jirani inayoongoza, ikiwa ni zaidi ya asilimia 30 ya mizigo yote.

Mtazamo kiuchumi

Uchaguzi huo unapaswa kuendeleza amani baina ya mataifa hayo kwa kuwa DR Congo ni turufu ya uchumi kwa Tanzania kama anavyofafanua mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania, Profesa Aurelia Kamuzora.

Mchumi huyo anasema DR Congo ni miongoni mwa nchi zisizo karibu na bahari, hivyo itaendelea kutumia zilizopo Tanzania iwapo amani na uhusiano baina ya nchi hizo itaendelea kuwepo.

"DRC ni moja ya nchi zisizo karibu na bahari (landlocked countries), wataendelea kutumia bandari zetu endapo tutaendelea kuwa na mahusiano mazuri na amani kama ilivyo kwa sasa," anasema.

Siri ya msisitizo wake wa amani katika uchaguzi huo ni kile alichokifafanua kuwa, amani ya Tanzania itaimarika zaidi iwapo majirani zake watakuwa na amani pia.

"Utulivu uliopo kwa sasa katika nchi za maziwa makuu unaongeza amani yetu. Endapo kutatokea vurugu huko kwa sababu ya uchaguzi, haitaathirika mifumo ya ugavi ya DRC tu, hata Tanzania pia," anaeleza na kuongeza:

"Pia ikumbukwe nchi hufanya biashara zaidi na nchi zilizo jirani kuliko nchi zilizo mbali. Hivyo ujirani wenye amani utakuza uchumi Tanzania," anasema.

Endapo kuna cha kuwafundisha DR Congo kuhusu uchaguzi wenye amani nchini mwao, anasema Tanzania inapaswa kuwa mstari wa mbele kufanya hivyo kwa kuwa ni jirani yake.

"Raia wa DRC wajitahidi kudumisha amani kwenye uchaguzi wakijifunza kutoka kwetu. Wajue baada ya uchaguzi kuna maisha na wafahamu pia kuwa viongozi wazuri hutokana na raia wenyewe.

Wajione sehemu ya uongozi wao, wasitegemee kuwa na kiongozi bora kama wenyewe hawamsaidii kiongozi huyo. Wakubali kuwa kiongozi anatokana na wao, hivyo atakayechaguliwa wamkubali ili wabaki na amani," anasema.

Uhusiano uendelezwe

Lakini, mchambuzi wa masuala ya uchumi na siasa, Gabriel Mwang'onda anasema uchaguzi huo unapaswa kuleta kiongozi atakayeendeleza uhusiano baina ya nchi hizo.

"Hatujui bado nani atashinda lakini yeyote atakayeshinda uhusiano wetu ni mkubwa kiuchumi na anapaswa kuuendeleza," anasema.

Anaeleza uchaguzi huo ndio utakaoamua ama kuongeza idadi ya mizigo ya DRC inayohudumiwa katika Bandari ya Tanzania au kupungua.

Hata hivyo, anasema matarajio yake makubwa ni kupatikana kiongozi atakayesimamia umaliziaji wa bandari ya Kalemie ambayo upande wa Tanzania tayari imeshakamilika.

Wakongo waliopo Tanzania

Majesté Kimpir ni raia wa DRC anayeishi nchini Tanzania kwa shughuli za biashara, anasema hatamani kuona uchaguzi huo unazorotesha uhusiano kati ya nchi hizo kibiashara na mambo mengine.

Anasema uhuru alionao wa kufanya kazi na biashara nchini Tanzania, umetokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya mataifa hayo, akisisitiza ni muhimu ikatafutwa mbinu ya kuendeleza sio kukatisha.

Kwa hali ilivyo, anasema kuna wasiwasi juu ya amani kuelekea uchaguzi huo kwa kuwa wananchi wanalalamika kukosekana kwa viongozi wenye uzalendo kama ilivyo Tanzania.

"Kule kwetu (DRC) viongozi wanapendekezwa na Ufaransa, hawana uzalendo na hata nchi yetu haina demokrasia kama ilivyo Tanzania, kwa maslahi ya uchumi na uhusiano wa kibiashara, uchaguzi unapaswa uwe na mfano wa huu wa Tanzania," anasema.

Uchaguzi huo pia, umemuibua Dekanto Bass raia wa Kongo anayefanya shughuli za muziki nchini Tanzania, anayesema amani ndiyo msingi wa kila kitu.

"Tukivuruga amani au akipatikana kiongozi atakayevuruga amani na majirani zetu, sisi hatutapata nafasi ya kuendelea kufanya kazi huku nje kama hivi. Viongozi wahakikishe kunakuwa na amani katika uchaguzi," anasema.

Undani kuhusu uchaguzi DRC

Huu utakuwa ni uchaguzi wa pili kuandaliwa kwa amani baada ya misukisuko ya kisiasa na mapinduzi ya serikali katika taifa la DRC.

Hata hivyo, uchaguzi huo unafanyika wakati DRC ikiwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani.

Inakadiriwa watu milioni 6.9 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mwaka 2022 kutokana na machafuko yanayoendelea.

Umoja wa Mataifa, unakadiria asilimia 28 ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao Kivu Kaskazini huku asilimia 39 wakihama Ituri.

Hatua hiyo imetokana na kukithiri kwa ghasia hasa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri nchini humo.

Si hivyo tu, makundi ya waasi yakiwemo M23, Allied Democratic Forces (ADF) na Codeco yanaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya raia na wanajeshi.

TRT Afrika