Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Uhifadhi wa tembo barani Afrika unatofautiana kulingana na malengo ya nchi. Uwindaji wa vitalu au Trophy Hunting unatumika kuwahifadhi nchini Tanzania.
Hii inahusisha serikali kutoa vibali vya uwindaji kwa makampuni na watu kulipia kuwinda wanyama hao.
Mamlaka ya Wanyamapori nchini Tanzania inatazamiwa kuamua kama itatoa vibali zaidi vya uwindaji wa vitalu wa wanyama pori kwa mwaka ujao huku kukuwa na ripoti ya kupungua kwa idadi ya tembo wakubwa, maarufu kama Super Tuskers.
Hawa ni tembo dume mwenye meno yenye uzito wa takriban kilo 45 kila moja ambayo hugusa chini pindi wanapotembea. Fahali pekee ndio wanaweza kuwa Super Tusker. Kwa Tanzania, ni tembo wanane tu waliosalia ndio wenye ukubwa huo.
Wanaharakati wanaonya kuwa kuwindwa kunatishia mustakabali wa idadi yao.Lakini kuna gharama ya kumtunza. Kila mwaka inaweza kugharimu $50,000.
Huku ada ya kuwinda tembo mkubwa nchini Tanzania inagharimu takriban dola 20,000, ila wahifadhi wanasema thamani ya maisha ya tembo wa kawaida kutoka kwa utalii inakadiriwa kuwa $1,607,625.
Wahifadhi wanasema kuwa inachukua miaka 35 kwa tembo dume kufikia ukubwa na uzoefu wa kuzaliana kila mwaka.
Lakini nchi jirani ya Kenya haitumii mbinu hii ya uhifadhi. Kenya ilipiga marufuku uwindaji wa fedha mwaka 1977 na inategema mapato kutoka kwa utalii peke yake. Hii inaleta changamoto ya hifadhi kwani nchi hizi mbili zina sera tofauti ilhali zinapakana.
Tembo hawa wakubwa huzunguka katika mandhari ya Amboseli-Magharibi ya Kilimanjaro inayopakana na Hifadhi ya Kitaifa ya Mlima Kilimanjaro na kuvuka mpaka wa Kenya na Tanzania.
Mwaka 2023 mvutano uliibuka wakati serikali ya Tanzania ilipomaliza mkataba usio rasmi wa miaka 30 na Kenya kwa kuruhusu wawindaji kuwapiga risasi kihalali angalau wawili kati ya 10 waliosalia.
Tukiangalia nchi kama Botswana uwindaji wa vitalu una sababu za kiusalama. Nchini humo kuna takribani tembo 130,000.
Ni wengi sana na imekuwa vigumu kwa serikali kuwahifadhi. Nchi hiyo ilipiga marufuku uwindanji wa vitalu wa tembo mwaka 2014 lakini ikaondoa marufuku hiyo mwaka 2019.
Hii ilikuwa baada ya jamii kulalamikia kwamba tembo ni wengi na wamekuwa tishio kwa maisha yao na mimea.
Nchi hiyo hata imejaribu kuwapuguza kwa kutoa tembo 8,000 kwa Angola na wengine 500 kwa Msumbiji bure.
Lakini sasa kuna msukumo kutoka nchi kama Marekani na nchi za ulaya kuwa uwindaji wa vitalu upigwe marufuku ili kupinga changamoto kama mauzo yasiyo halali ya meno ya tembo, na kupunguka kwa kasi kwa idadi ya wanyama.