Uturuki imetoa rambirambi kwa Uganda baada ya shambulio la kigaidi Ijumaa usiku dhidi ya shule ya upili magharibi mwa nchi. Ripoti zaonyesha kuwa maiti 41 zimepatikana.
Mashambulizi yalifanywa na kundi la waasi la Allied Democrratic Forces, ADF.
"Tumesikitishwa sana na wanafunzi wengi kupoteza maisha yao katika shambulio hilo, na tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na tunawatakia afueni ya haraka majeruhi," Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake.
"Uturuki, nchi inayopigana kwa uthabiti dhidi ya aina zote za ugaidi, inasimama na serikali na watu wa Uganda katika siku hii ngumu," iliongeza.
Mkurugenzi eneo la mpaka la Mpondwe-Lhubiriha, Selevest Mapoze alisema maiti 41 zilitolewa katika shule hiyo na 38 kati yao ni wanafunzi.
Awali, msemaji wa jeshi Brig. Jenerali Felix Kulayigye katika taarifa alisema kuwa idadi ya waliokufa imeongezeka hadi 37 baada ya miili mingine 12 kugunduliwa.
Alisema baadhi ya miili hiyo iliteketea kwa moto kiasi cha kutotambulika na mamlaka itatumia vipimo vya DNA ili kubaini utambulisho wao. Aliongezea kuwa waasi pia waliwateka nyara wanafunzi sita,
Ubalozi wa Uturuki nchini Uganda pia umelaani shambulizi la kigaidi lililolenga shule hiyo.
“Nimesikitishwa sana na tukio la kigaidi lililotokea katika shule ya sekondari Lhubirira iliyopo Mpondwe usiku wa kuamkia jana. Kulenga watoto ni kitu kisichoeleweka. Ninalaani vikali shambulio hili mbaya na ninatuma rambirambi zangu kwa familia za wahasiriwa," Balozi wa Uturuki nchini Uganda, Mehmet Fatih Ak alisema katika mtandawo wa twitter.
Awali, katika taarifa yake, msemaji wa polisi wa Uganda, Fred Enanga alisema kuwa baada ya kuwaua wanafunzi hao katika wilaya ya Kasese, waasi wa ADF walipora mali pamoja na chakula kabla ya kuchoma mabweni ya shule hiyo.
Waasi wa ADF walitoka magharibi mwa Uganda mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa nia ya kupindua utawala wa Rais Yoweri Museveni lakini walizidiwa nguvu na jeshi la Uganda.
Walikimbilia msituni Mashariki mwa DR Congo, ambapo mara nyingi hushambulia vijiji na kuua watu.
Jeshi la Uganda linasema baada ya mashambulizi walikimbilia mbuga ya wanyama ya Virunga nchini DRC ambapo jeshi la Uganda na polisi wamewafuata kuwasaka.