Mnamo Februari 2024, Uganda ilipitisha bajeti ya Dola za Kimarekani 886, 998 kwa nia ya kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika eneo la Afrika Mashariki.
Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi za Afrika Mashariki, EAC.
Kifungu cha 137 cha Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya EAC, kinagusia kuendelezwa kwa lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Uganda bado haijaunda baraza hilo.
Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among ameitaka serikali ya nchi hiyo kuweka wazi iwapo muswada wa Baraza la Kiswahili la Taifa wa 2024 ni halisi kwani haukuwa na sahihi ya waziri wa Jinsia.
Hii ni baada ya kubainika kuwa muswada huo uliwasilishwa bila saini ya Waziri wa Jinsia, Betty Amongi.
“Pia kulikuwa na kipengele cha mtu kufadhili muswada huo na kuutuma bila saini. Je, tunathibitishaje kama muswada huo ni halali, ama la.”
Mwakilishi wa jimbo la Maracha, Denis Oguzu ametoa notisi ya mdomo tu , akitishia kuliburuza bunge hilo mahakamani iwapo litaendelea na kupitisha Muswada wa Kitaifa wa Kiswahili wa 2024, bila ya uwepo wa sahihi ya Betty Amongi.
" Ni vyema waziri atoe hoja ya kuuondoa Muswada huu ili uletwe kwa njia ya halali. Vinginevyo, tukiendelea na muswada huu, lazima ujiandae kwa changamoto ya kisheria na hii ni notisi kwa bunge,” alisema Oguzu.
Hata hivyo, wabunge wengine walipinga mpango wa kuwa na baraza la Kiswahili nchini Uganda.
“Sikubaliani na wazo zima la kuunda Baraza. Tunasoma Kiingereza na nyie wote hapa mnaongea Kiingereza, kuna Baraza la Kiingereza? Unaongea lugha yako, luganda na kadhalika , huwezi kuwa Bunge lile lile linalounga mkono hoja na ukaruhusu Serikali kwa uvivu, ianze kuunda Baraza. “ alieleza Ssemujju Nganda, mbunge wa eneo la Kira.
"Sijui Serikali hii inafanyaje kazi, tunapaswa kumshukuru Mungu kwamba bado tupo. Kwa sababu ukitaka kueneza lugha, ijulishe tu na ifanye iwe ya lazima shuleni. Una watoto milioni 12 ambao wako Shule za Msingi, kwa nini unalisumbua Bunge mchana mzima kujadili kuundwa kwa Baraza, kwa madhumuni ya kukuza lugha? " Nga'nda alihoji.
Mnamo mwaka wa 2017, Baraza la Mawaziri la EAC liliagiza nchi wanachama zianzishe mchakato wa kukifanya Kiswahili kama lugha rasmi ya Afrika Mashariki, kupitia uanzishwaji wa Mabaraza ya Taifa ya Kiswahili.
Kenya haijaanzisha Baraza la Kiswahili la Taifa - Baraza la Kiswahili la Kenya (Bakike) kulingana na matakwa ya EAC.
Hadi sasa, ni Tanzania pekee iliyoanzisha baraza lake, liitwalo Baraza la Kiswahili la Tanzania (Bakita), lililoanzishwa mwaka 1967.