Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan (katikati), Waziri wa Mambo ya Nje wa EthiopiaTaye Atske Selassie (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi (kulia) wakiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Ankara . Picha: AA

Na Emmanuel Onyango

Mazungumzo yaliyoratibiwa na Uturuki, yenye nia ya kutafuta suluhu kati ya Ethiopia na Somalia yanaashiria dalili njema, hasa baada ya miezi mingi ya kuhitilafiana kidiplomasia kutokana na mkataba tata wa bandari kati ya Ethiopia na eneo lililojitenga la Somaliland.

Mwanzoni mwa mwaka 2024, Ethiopia na Somaliland zilitangaza kuwa zimetiliana sani hati ya makubaliano yenye kuiruhusu Ethiopia kutumia Bahari Nyekundu, na pia kuitambua Somaliland kama taifa huru.

Ethiopia ni isiyokuwa na chanzo chochote cha maji na inajulikana kwa wingi wa idadi ya watu. Mwaka 1993, nchi hiyo ilipoteza hadhi ya kuwa na Bahari Nyekundu baada ya kujiondoa kwa Eritrea.

Nchi hiyo imekuwa ikitumia bandari iliyo karibu na nchi ya Djibouti kwa ajili ya biashara ya ndani na nje, huku Waziri Mkuu Abiy Ahmed, akisisitiza umuhimu wa kuwa na bahari.

Kutafuta suluhu

Somalia, ambayo inaichukulia Somaliland kama sehemu yake, ililaani mpango huo, ikiuita kuwa ni ukiukwaji wa mamlaka yake na uadilifu wa eneo. Pia, inaishutumu Ethiopia kwa tamaa ya kunyakua sehemu ya Somalia, jambo ambalo Addis Ababa inakanusha.

Umoja wa Afrika na mataifa yenye nguvu duniani yaliunga mkono wito wa kutaka haki ya Somalia iheshimiwe, huku wakisisitiza suluhu kupitia mazungumzo.

Jitihada za kupunguza uhasama kati ya nchi hizo mbili majirani ziligonga mwamba.

Hivi karibuni, Uturuki iliingilia kati suala hiloKatika hatua ya hivi punde ya kumaliza mgogoro huo, ikiwa kama msulihushi mkuu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan aliwakaribisha mawaziri wenzake wa Ethiopia na Somalia mjini Ankara siku ya Jumatatu na kujadili njia za kutatua tofauti zao "ndani ya mfumo unaokubalika."

“Utayari wetu katika kuleta amani, diplomasia na nia yetu njema ,”Fidan aliwaambia waandishi wa habari jijini Ankara, mbele ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia na Somalia baada ya mazungumzo hayo.

'Msuluhishi wa asili'

Serikali ya Somalia hapo awali ilisema kwamba ingeingia tu katika mazungumzo kuhusu mpango wa bandari baada ya Ethiopia kushutumu mpango wake na Somaliland na kuomba radhi hadharani.

Uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na nchi hizo mbili unachukuliwa kuwa jambo la muhimu katika kufikia mafanikio yoyote katika mazungumzo hayo.

Pande hizo zimekubaliana kukutana mjini Ankara mwezi Septemba katika duru ya pili ya majadiliano.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Pembe ya Afrika wamepongeza mpango wa kidiplomasia wa Uturuki.

“Hatuna budi kuzipongeza serikali za Ethiopia na Somalia kwa nia yao thabiti ya kupoza mizozo ya kidiplomasia,” amesema Nuur Mohamud Sheekh, msemaji wa zamani wa Mkurugenzi Mtendaji wa nchi za IGAD.

"Sifa zote ziende kwa Uturuki kwa kuwezesha mazungumzo haya muhimu," aliiambia TRT Afrika.

Ni mapema sana kuzungumzia njia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya majirani wa Pembe ya Afrika japo bado tuna matumaini na nafasi ya Ankara katika mchakato huu.

"Uturuki ina uhusiano mzuri na serikali zote mbili na (Waziri Mkuu wa Ethiopia) Abiy na Rais Hassan (wa Somalia),'' alisema Mohamud.

Na ndio maana mchambuzi huyo akailezea Uturuki kama mpatanishi wa asili, mwenye kuaminika.

Ushirikiano wa kimkakati

"Ninaamini ukweli kwamba mawaziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Ethiopia na Somalia wamekubali kukutana tena mwezi Septemba ni kielelezo cha nia ya kutatua hali hiyo," aliongeza.

Eneo la kimkakati la Somalia linachukuliwa kuwa na umuhimu mkubwa kutokana na upatikanaji wake wa Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

Mwezi uliopita ilipata nafasi ya muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uturuki ni kati ya washirika wakubwa wa Somalia tangu Rais Recep Tayyip Erdogan alipotembelea Mogadishu mwaka wa 2011. Uturuki mekuwa ikitoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Somalia na kutoa msaada wa maendeleo.

Uturuki na mawaziri wa ulinzi wa Somalia walitia saini makubaliano ya ushirikiano wa miaka 10 mwezi Februari ili kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na utulivu wa eneo hilo.

Uturuki imejenga shule, mahospitali na miundombinu na hata kutoa nafasi za masomo kwa Wasomali kusomea nchini Uturuki.

‘Bado tuna matumaini’

Ethiopia ni moja ya nchi za Kiafrika zenye uhusiano mkubwa wa kiuchumi na kidiplomasia na Uturuki.

Wachambuzi wanaamini kuwa kusuluhisha mvutano kati ya Somalia na Ethiopia ni muhimu kwa utulivu na maendeleo ya Afrika Mashariki na kwingineko, kutokana na changamoto nyingi za usalama na kiuchumi zilizopo katika eneo hilo.

Baadhi ya wataalam wanasema kutatua mvutano kati ya nchi hizo mbili ni kazi ngumu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan pia alikiri ''hali tata ya mienendo mingi itazingatiwa.''

Hata hivyo, alionekana mwenye matumaini. Duru ya kwanza ya mazungumzo ilikuwa ‘’iliruhusu pande zote mbili kueleza hisia zao kwa undani na kuwezesha pande zote kupata maelewano bora,’’ Fidan alisema.

‘’Bado tuna matumaini na siku sijazo,’’ aliongeza.

TRT Afrika