Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Mi mmasai bwana nasema mi masai,
Hayo ni baadhi ya maneno yanayopatikana katika wimbo uliotungwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, na msanii Mr Ebbo kutoka Tanzania.
Katika wimbo huo, msanii huyo ambaye kiasili ni Mmasai wa kutoka eneo la Longido, linalopatikana Arusha nchini Tanzania, anajivunia na kujisikia fahari kutokea kabila hilo.
Mr Ebbo, ambaye kwa sasa ni marehemu, anakwenda mbali zaidi na kudai hiyo Wamasai ndio tamaduni asilia, yenye nguvu iliyobaki Afrika.
Wakati dunia ulimwengu unaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu wa Kiasili Agosti 9, madai ya Mr Ebbo bado yanabaki kwenye mizania.
Hii inatokana na hoja kuwa, Wamasai, haswa wanaopatikana nchini Tanzania, sio watu wa kiasili.
Hoja hiyo haiwahusu Wamasai peke yake, bali hata jamii ya Wahadzabe wanaodhaniniwa kuwa wameishi kaskazini mwa Tanzania, wakila matunda na mizizi, na aina mbalimbali za wanyama kwa miaka 40,000.
"Ili watu fulani waidhinishwe kuwa wa asili ya eneo fulani ni lazima wafikie vigezo kadhaa vikiwemo vya Kiijografia, majina ya maeneo, shughuli za kiuchumi na ushahidi wa mabaki," mtaalamu wa mambo kale kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt Agness Gidna, anaiambia TRT Afrika.
Kulingana na mtaalamu huyo, uwingi wa watu wa jamii fulani katika eneo moja, haliwapi sifa ya kuwa watu wa asili wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa Dkt Gidna, eneo la Engaruka lililopo kaskazini mwa Tanzania, lifahamika sana kutokana na uwepo wa magofu ya kale.
"Inasadikiwa kuwa zaidi ya miaka 500 iliyopita, kulikuwa na jamii ya wakulima iliyotumia mfumo wa hali ya juu wa wa kilimo cha umwagiliaji, hata hivyo watu wanaoishi eneo hilo leo, wengi ni Wamasai, na sababu hiyo haiwafanyi wao kuwa jamii ya asili ya eneo husika," anasisitiza.
Isitoshe, Wamasai wanafahamika sana kwa ufugaji wa kuhamahama, na sio kilimo.
Kulingana na mtaalamu huyo wa mambo kale, Tanzania inafahamika kwa kuwa na jamii nne za Wakushi, Wanailot, San na Wabantu, na kwamba hakuna jamii yenye kudai kuwa ya asili.
"Ni ngumu kusema kuwa Wamasai ni watu wa asili ya Ngorongoro, kwani kumekuwepo na Wadatoga ambao wameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 400 iliyopita," anaeleza.
Dkt Gidna anasisitiza kuwa Tanzania haina jamii za asili, kwani makabila mengi yamekuwa yakihama kutoka eneo moja hadi nyingine, ambao umesababisha mtawanyiko wa watu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
"Tanzania inafahamika kuwa na lugha zaidi ya 126, kwahiyo hatuna jamii za asili."
Hoja hiyo inaungwa mkono na Engelbert Aloyce, mwenyekiti wa waongoza utalii nchini Tanzania.
"Tanzania haina jamii za asili, ila ina makabila yanayodumisha tamaduni zao kama vile Wahadzabe, Wadatoga na Wamasai," anasema.
Hata hivyo, kulingana na Aloyce, makabila haya yako hatarini kupoteza asili zao kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, utandawazi na kadhalika.
Hii ni tofauti sana, na nchi jirani ya Kenya, nchi inayosifika kwa kukumbatia ukabila.
Mfano mwa jamii ambazo zinadaiwa kuwa za asili nchini humo ni pamoja na Waogiek, ambayo inaaminika kuwa ndio jamii kubwa zaidi kati ya jamii zilizosalia ambazo maisha yazo ya kiuchumi ni uwindaji na uchumaji wa vyakula katika misitu.
Tayari jamii ya Waogiek wamejitambulisha kama jamii asilia, ili haki zao zitambuliwe na kulindwa inavyostahili kulingana na sheria za kimataifa, na hasa kama inavyotambuliwa na Mkataba wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na za Mataifa (AfCHPR), iliyoko Arusha nchini Tanzania.
Mwaka 2017, mahakama hiyo iliitaka serikali ya Kenya kutoiondoa jamii ya Ogiek msituni.
Mahakama hiyo iliitaka serikali ya Kenya, isifikirie kuiondoa jamii hiyo ndani ya msitu huo kwa sababu ndio ardhi yao ya asili.
Kwa sasa, Waogiek wanapatikana katika miinuko ya Mau na Aberdare mkoani Bonde la Ufa, na pia katika maeneo machache ya Mlima Elgon magharibi mwa Kenya.
Katika sehemu ya Afrika ya kati, kuna kabila la asili linaloishi kwenye kanda hiyo.
Mbilikimo ni kabila la watu wafupi barani Afrika, pia kwa kiingereza wanaitwa kabila la (Nigrillo), kwa wastani watu wazima wa kabila hilo wana urefu wa mita 1.3 hadi 1.4. Ingawa mbilikimo ni wafupi, lakini wana nguvu kubwa na wote ni wawindaji hodari na kujiita kuwa "watoto wa misitu".