Ukraine kuanzisha kitovu cha nafaka katika Bandari ya Kenya ya Mombasa

Ukraine kuanzisha kitovu cha nafaka katika Bandari ya Kenya ya Mombasa

Rais wa Kenya William Ruto atoa tangazo baada ya kukutana na rais wa Ukraine
Rais Ruto alikutana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy mjini New York / Picha kutoka William Ruto

Rais wa Kenya William Ruto, alitangaza Jumanne kwamba Ukraine itaanzisha kitovu cha nafaka nchini mwake katika hatua muhimu ya kukabiliana na uhaba wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki.

Rais Ruto alitamka uamuzi huo kufuatia mazungumzo yake na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy mjini New York, ambapo viongozi hao wawili wanahudhuria Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake, Ruto alisema, "Nimefanya mazungumzo na Rais wa Ukraine Zelenskyy, ambaye alijitolea kuanzisha kituo cha nafaka katika Bandari ya Mombasa ili kukabiliana na uhaba wa chakula Afrika Mashariki."

Ukraine, inayotambuliwa kama nchi yenye nguvu duniani katika uzalishaji wa nafaka muhimu, inatarajiwa kuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula katika kanda ya Afrika Mashariki.

Uhaba wa chakula

Mazimio kati ya Kenya na Ukraine yanalenga kukabiliana na tatizo linaloendelea la uhaba wa chakula ambalo limechangiwa na mambo mbalimbali, yakiwemo mabadiliko ya tabia nchi, kuyumba kwa kisiasa na kukatika kwa minyororo ya ugavi duniani.

Kuanzishwa kwa kitovu cha nafaka katika Bandari ya Mombasa kunatarajiwa kurahisisha uingizaji na usambazaji mzuri wa nafaka, kuhakikisha usambazaji wa chakula thabiti na wa kutegemewa kwa mataifa ya Afrika Mashariki.

Kufuatia vita kati ya Urusi na Ukraine kuanza mnamo Februari 2022, kumekuwa na uhaba wa nafaka katika masoko ya kimataifa ya nafaka, ambayo yamepunguza usambazaji wa chakula katika mikoa inayotegemea nafaka ya Ukraine.

Rais Ruto alieleza kujitolea kwa nchi yake kutetea suluhu la amani kwa mzozo wa Urusi na Ukraine.

TRT Afrika