Takriban watu milioni 68 Kusini mwa Afrika wanakabiliwa na ukame uliosababishwa na El Nino, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imesema Jumamosi.
Ukame huo ulioanza mwanzoni mwa mwaka 2024, umeathiri uzalishaji wa mifugo na mazao, na hivyo kusababisha upungufu mkubwa chakula.
Wakuu wa nchi 16 za SADC wanakutana jijini Harare, Zimbabwe kujadili hali ya usalama wa chakula katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi asilimia 17 ya watu katika ukanda huo wana uhitaji wa misaada..
Uzalishaji wa hewa chafu
“Msimu wa mvua wa 2024 umekuwa na changamoto nyingi huku sehemu nyingi za ukanda huu zikikumbwa na athari mbaya za hali ya El Nino inayodhihirishwa na kuchelewa kuanza kwa mvua,” alisema.
Nchi zikiwemo Zimbabwe, Zambia, na Malawi tayari zimetangaza janga la njaa kuwa hali ya maafa, huku Lesotho na Namibia zikitoa wito wa msaada wa kibinadamu.
Misaada ya haraka
Ukanda huo ulituma maombi ya dola bilioni 5.5 mwezi Mei kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kukabiliana na ukame, lakini maombi hayo hayajajibiwa, alisema mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake Joao Lourenco, Rais wa Angola.
"Kiasi kilichopatikana hadi sasa hakitoshi na niombe kuwasisitizia washirika wetu wa maendeleo kuendelea kutusaidia," aliuambia mkutano huo.
Janga la ukame ni ajenda iliyotawala mkutano huo, sambamba na masuala kama vile mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.