Nchini Kenya, maafisa waliripoti kuongezeka kwa Uhalifu wa Mtandaoni kunakadiriwa kufikia zaidi ya visa bilioni moja katika robo ya mwisho ya 2023 pekee. / Picha: Getty Images

Na Dayo Yussuf

TRT Afrika, Istanbul

Uhalifu mtandaoni si jambo jipya. Watu wengi ama wamedhulumiwa au angalau wanamjua mtu ambaye amedhulumiwa mtandaoni kwa njia moja au nyingine.

Lakini kasi ambayo uhalifu wa mtandaoni umebadilika ni sababu ya wasiwasi sio tu kwa watu binafsi lakini mashirika na mashirika na taasisi za serikali pia.

‘’Tumekuwa tukiona ongezeko kubwa la uhalifu mtandaoni lakini pia aina za uhalifu na walengwa pia.’’ Anasema Yusuph Kileo, mtaalamu wa Uhalifu wa Mtandao na mchambuzi wa uhalifu wa kidijitali nchini Kenya. ‘’Hata pamoja na hayo, bado hatuna picha halisi kwani uhalifu mwingi hauripotiwi,’’ Yusuph anaiambia TRT Afrika.

Nchini Kenya, maafisa waliripoti kuongezeka kwa Uhalifu wa Mtandaoni kunakadiriwa kufikia zaidi ya visa bilioni moja katika robo ya mwisho ya 2023 pekee.

Ikilinganishwa na visa milioni 123 vilivyoripotiwa katika robo iliyotangulia, hii inatoa picha mbaya ya mustakabali wa usalama wa Mtandao nchini.

Kufuatia takwimu hizo, wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ICT ilitangaza hatua kali kote nchini.

‘’Serikali inaboresha mifumo yake ya kutambua vitisho, na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kukabiliana na vitisho hivyo,’’ Edward Kisiang’ani, katibu mkuu wa Matangazo na Mawasiliano alisema. ‘’ Wizara ina nia ya "kushirikiana na nchi katika kanda katika kupunguza matishio ya mitandao ya mipakani." Aliongeza.

Kadiri tunavyosisimka katika ukuaji wa muunganisho tunahitaji kufahamu kuwa inakuja na ongezeko la hatari ya wizi, ulaghai na uhalifu mwingine unaohusiana na mtandao.

Kadiri tunavyozidi kutegemea teknolojia ya kisasa ndivyo tunavyozidi kukabiliwa na mashambulizi ya mtandaoni ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa usalama katika viwango vya ushirika.

Wahalifu wa kimtandao wamekuwa wakilenga mashirika na taasisi za fedha / Picha : Getty 

Wahalifu wa mtandao pia wanaboresha kila mara ili kukwepa juhudi zote za kuwaweka nje na mikakati bora, rasilimali na ujuzi. Ikiwa hazitasonga kwa kasi sawa, serikali nyingi zitajikuta zikicheza na wahalifu.

‘’Uhalifu wa mtandaoni haubagui, hauchagui. Lakini tumeona walengwa fulani ambao wanaathiriwa zaidi. Kwa mfano kuna wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya taasisi za fedha kama mabenki,’’ mchambuzi wa kidijitali Yusuph anaiambia TRT Afrika. ‘’Lakini pia tunaona wazee waliostaafu wakilengwa hasa mtandaoni ambapo wanapoteza akiba zao z amaisha. Pia hospitali zimekuwa mteremko kwa wahalifu wanaokuja kuvuna data za kibinafsi katika nchi nyingi za Afrika,’’ Yusuph anaeleza.

Lakini baadhi ya data za kutisha zaidi zinaelekeza kwa watoto kama wahasiriwa walio katika hatari kubwa ya uhalifu wa mtandaoni.

Tanzania kwa mfano imekuja na sera ya kimkakati dhidi ya uhalifu wa mtandaoni /Picha : Getty 

Zaidi ya kulaghaiwa kupoteza pesa, wengine wanaonewa kwenye ponografia ya mtandaoni au ulanguzi wa binadamu.

‘’Wazee hawa au watoto wanalengwa kwa sababu wana uelewa mdogo wa uhalifu mtandaoni,’’ Yusuph anasema.

Tanzania kwa mfano imekuja na kamati maalum ya ushauri wa usalama wa mtoto mtandaoni na kampeni maalum ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto mtandaoni.

Mkakati huo utajaribiwa kwa muda wa mwaka mmoja, baada ya hapo watatathmini na kuamua sera ya muda mrefu.

Mkakati unalenga kulenga masuala makuu matatu:

  • 1. Uhamasishaji nchini kote - Serikali zinalenga kutoa uhamasishaji nchini kuhusu usalama wa watoto mtandaoni, kwa watoto na walezi wao.

  • 2. Pia sera za nchi zinazoshughulikia Uhalifu wa Mtandaoni zitabainisha uhalifu mkuu unaolenga watoto mtandaoni na kurekebisha sheria, mikakati na michakato muhimu ya kuwalinda watoto.

  • 3. Kuweka ulinzi wa kifaa - Watoto wengi sasa wanaweza kufikia vifaa vya kielektroniki viwe vimeundwa kwa ajili ya watoto au watu wazima lakini vinaruhusiwa kutumiwa na watoto, kwa hivyo serikali inalenga kusakinisha teknolojia ya ulinzi katika vifaa hivi ili kudhibiti jinsi na kile ambacho watoto hufanya mtandaoni.

Kulingana na wataalamu, hata vijana wenye uzoefu wa teknolojia na mtandao hawajasalimika.

Uhalifu wa mtandaoni hauhusiani na eneo mahususi. Hautambui aliko mwathiriwa au mlengwa na unafikia nchi zote. / Picha : Getty 

‘’Tunaona vijana hawa wanaofanya biashara mtandaoni kwa kutumia sarafu za crypto wakilalamika kuwa wamepoteza pesa zao zote kwa biashara ghushi au kupotoshwa na kutumia pesa zao zote,’’ anasema Yusuf. ''Pia wale wanaofanya kazi mtandaoni au kuwa na biashara za mtandaoni wanalengwa,’’ anaongeza.

Nchi nyingi zina sheria zinazotumika kupambana na Uhalifu wa Mtandao mbalimbali. Hata hivyo wataalam wanasema sheria hiyo inakuwa changamoto katika utekelezaji.

''Hata hivyo sheria ni kali, sheria sio muarubaini kwa uhalifu,'' Yusuf anaiambia TRT Afrika. ''Kama una sheria lakini wananchi hawaielewi, au wanaoitunga hawajapewa uwezo wa kutosha kukabiliana na changamoto, ukiwa na sheria lakini hakuna ushirikiano au ushirikiano ni mdogo sana, basi sheria haiwafai,'' anaomgeza.

Uhalifu wa mtandaoni hauhusiani na eneo mahususi. Hautambui aliko mwathiriwa au mlengwa na unafikia nchi zote.

Kwa sababu hiyo wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano kamili sio tu kati ya mashirika ndani ya nchi lakini inapaswa kuvuka mipaka kati ya nchi, haswa kushiriki habari za kijasusi, kwa matokeo bora katika ulinzi wa Uhalifu wa Mtandao.

Epuka kutumia programu ambazo huzifahamu au hujui ni data gani ya kibinafsi inakusanya kutoka kwako na ikiwa huihitaji, usijisajili.  / Picha : Getty 

Kwa hivyo unaweza kufanya nini ili kujikinga na uhalifu wa Mtandao?

Kwanza kabisa ni muhimu kutambua kuwa wewe ni mlinzi wako na jukumu kuu la kujilinda na data yako ni lako.

Wataalamu wanashauri jinsi ya kujikinga vyema

  • Kuwa na manenosiri yanayofaa na thabiti ya vifaa vyako vyote lakini pia usiishiriki na wengine au kutumia herufi ambazo ni rahisi kukisia.

  • Unapojiunga mtandaoni, tulia, kisha fikiria. Fikiri kabla ya kubofya viungo vilivyotumwa kwako

  • Epuka kutumia programu ambazo huzifahamu au hujui ni data gani ya kibinafsi inakusanya kutoka kwako na ikiwa huihitaji, usijisajili.

  • Pia angalia mipangilio yako ya faragha na uhakikishe kuwa unalinda maelezo yako ya kibinafsi kama vile tarehe ya kuzaliwa kwa kuwa yanaweza kutumika kukusanya data zaidi ya kibinafsi.

TRT Afrika